Tume ya Ushindani na Haki (FCC) nchini imeteketeza vipuri bandia vya magari, na kuwaonya wafanyabiashara kujiepusha kununua na kuuza bidhaa zilizoghushiwa.

Shughuli ya uteketezaji huo imefanyika hivi karibuni katika tanuri la Kiwanda cha Chuma kinachojulikana kama MMI Steel Mills kilichopo Mwenge, Dar es Salaam, chini ya usimamizi wa Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Mkoni, miongoni mwa maofisa wengine wa jeshi hilo.

 

Afisa Mwandamizi wa Mawasiliano na Uhusiano wa Umma katika FCC, Frank Mdimi, amesema vipuri hivyo vilikutwa na nembo ya AK iliyoghushiwa.

 

“Vipuri hivi vimekamatwa na Tume ya Ushindani kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, katika msako uliofanyika eneo la Kariakoo, Dar es Salaam, kati ya Januari 24 na Februari 1, mwaka huu,” amesema Mdimi.

 

Vipuri hivyo vinahusisha seti 1,199 za ‘Brake Pads’ na seti 11 za ‘Drum Brake Shoes’ zilizokamatwa katika maduka manne yanayomilikiwa na watu tofauti eneo la Kariakoo.


“Ukaguzi huo umefanywa baada ya Tume kupokea malalamiko kutoka kwa mmiliki halali wa nembo ya AK, Kampuni ya Al Khair Auto Parts ya Dubai, Falme za Kiarabu, iliyobaini kuwapo kwa wafanyabiashara wanaotumia nembo hiyo bila ruhusa yake na hivyo kuharibu soko lake, hasa kwa kuwa bidhaa zinazoghushiwa ni hafifu,” amefafanua Mdimi.


Wakati vipuri halisi vya AK hutengenezwa kwa metali pekee, vipuri hivyo bandia vimebainika kutengenezwa na malighafi nyingine iliyoongezwa kwenye metali na kuvifanya kutokuwa madhubuti, tofauti na vilivyo halisi.

 

Mkuu wa Idara ya Udhibiti wa Bidhaa Bandia katika FCC, John Mponela, ameyataja maduka yaliyokutwa na vipuri hivyo kuwa ni Several Auto Spare Parts, Aisin Auto Parts, Nassoro Chande Nassoro na Mohamed Ibrahim Ratansi.

 

Wamiliki wa maduka hayo, kwa mujibu wa Mponela, wamekwishaadhibiwa na Tume hiyo kwa kutozwa faini ya fedha taslim na kugharamia uteketezaji wa vipuri hivyo.

 

Kufuatia tukio hilo, Mdimi amewataka wafanyabiashara na wananchi kwa jumla, kujiepusha na ununuzi holela wa bidhaa  kwani kufanya hivyo kunawaweka katika hatari ya kununua zilizoghushiwa kinyume cha sheria za nchi.

 

Badala yake, amewahimiza kuhakikisha wananunua bidhaa kutoka kwa wasambazaji waliohalalishwa kisheria, ili pia iwe rahisi kuwasilisha malalmiko yao endapo matatizo yatajitokeza katika matumizi ya bidhaa husika.

 

Kwa upande mwingine, Mponela amekumbusha kuwa kwa sasa sheria imeongezwa makali, na hivyo kuwataka wananchi kuacha kujihusisha na biashara ya bidhaa bandia ili kuepuka kukabiliwa na adhabu kali.

 

Sheria inasema adhabu ya mtu anayeuza bidhaa bandia ni kutozwa faini isiyozidi Sh milioni tano, kupokonywa bidhaa husika na kugharamia uteketezaji wa bidhaa hizo.

 

Hata hivyo, FCC imeendelea kutoa wito kwa wasambazaji wa bidhaa mbalimbali, kuhakikisha wanalinda hatimiliki bunifu ya bidhaa zao ili zisighushiwe, lakini pia wajenge dhana ya kuwaelimisha wananchi kuhusu ubora wa bidhaa zao, nembo wanazotumia na namna ya kujihadhari na bidhaa bandia.


Please follow and like us:
Pin Share