Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mbeya

JESHI la Polisi mkoani Mbeya kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kupambana na Kuzuia Dawa za kulevya (DCEA) wamekamata gari likiwa limebeba shehena ya dawa za kulevya aina ya bangi zikiletwa nchini kutoka Malawi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga alibainisha hayo mwishoni mwa wiki wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu operesheni zinazofanywa na jeshi hilo.

Kamanda Kuzaga alisema gari hilo lilikamatwa katika Wilaya ya Rungwe baada ya kupata taarifa za siri kutoka kwa baadhi ya watu kuwa gari hilo lilikuwa limebeba dawa za kulevya.

Alilitaja gari lililokamatwa kuwa ni Mitsubishi Canter lenye namba za usajili T 833 EDN na kwamba lilikuwa limebeba vifurushi 67 vya dawa hizo likitokea Malawi kuingia nchini kupitia mpaka wa Kasumulu wilayani Kyela.

Alisema, awali gari hilo lilikuwa linajulikana kuwa lilikuwa limebeba magunia ya pumba za mpunga kwa ajili ya mifugo, lakini baada ya kulifanyia upekuzi walibaini kuwa magunia ya pumba yalikuwa machache na yaliwekwa mwanzoni ili kuzuia bangi zisionekane.

“Baada ya kushusha magunia ya pumba tulikuta vifurushi 67 vya bangi, tunakusudia kushirikiana na mamlaka nyingine kupima ili kujua dawa hizo zilikuwa na uzito gani, pia tutapeleka kwa mkemia mkuu wa serikali kupima sampuli,” alisema Kuzaga.

Mjumbe wa Serikali ya Kitongoji cha Kawetere wilayani Rungwe mahali gari hilo lilipokamatwa, Julius Tweve alisema alishuhudia wakati upekuzi unafanyika kwenye gari hilo na aliona shehena ilivyokuwa kubwa na kwamba endapo mzigo huo ungesambazwa mitaani ungeleta athari kwa vijana wengi.