Italia imetangaza siku tano za maombolezo ya kitaifa kufuatia kifo cha kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, huku bendera ikipeperushwa nusu mlingoti kwenye majengo yote ya umma. Viongozi mbalimbali wa dunia wametangaza kushiriki maziko ya kiongozi huyo wa kiroho siku ya Jumamosi.

Hali ya usalama imeimarishwa katika mji mkuu wa Italia, Roma kabla ya ibada ya mazishi na maziko ya Papa Francis aliyefariki Jumatatu, yatakayofanyika  siku ya Jumamosi. Viongozi wa ngazi za juu kutoka nchi mbalimbali za ulimwengu wanatarajiwa kushiriki.

Rais wa Halmashauri Kuu wa Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen pamoja na Rais wa Baraza la Ulaya Antonio Costa, ni miongoni mwa waliothibitisha kushiriki mazishi hayo yatakayofanyika kwenye kanisa la Mtakatifu Maria Mkuu ambalo liko karibu na kituo kikuu cha treni mjini Roma, kilomita chache kutoka Vatican.

Msemaji wa Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, Arianna Podesta akitowa salamu za rambirambi za kiongozi huyo alikuwa na haya.

Ulimwengu unaomboleza kifo cha Papa Francis, aliwavutia mamilioni ya watu zaidi ya kanisa Katoliki kutokana na unyenyekevu na upendo wake wa kweli kwa wasiojiweza. Mawazo yetu yako pamoja na wote waliopoteza. Wapate faraja kupitia urithi wa Papa Francis utakaoendelea kuishi na kutuongoza sote kuelekea ulimwengu wa haki, amani na huruma. Pia nithibitishe kwamba Rais von der Leyen, atashiriki Jumamosi shughuli ya mazishi ya Papa Francis”

Bendera pia zimeshushwa nusu mlingoti katika makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels kumuenzi. Miongoni mwa viongozi wengine wa dunia waliothibitisha kushiriki mazishi ya Papa Francis ni pamoja na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na Rais Frank Walter Steinmeier ambaye ndiye atakayeongoza ujumbe wa viongozi kutoka Ujerumani.

Rais Volodymr Zelensky wa Ukraine, na Rais Donald Trump wa Marekani pia wamethibitisha kwenda Roma huku ikulu ya Urusi, Kremlin ikitangaza kwamba Rais Vladmir Putin hatokwenda, na hivyo kuzima minong’ono kwamba kiongozi huyo huenda akashiriki mazishi hayo licha ya kuwepo waranti wa kimataifa wa kutaka akamatwe. Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, amesema bado haijaamuliwa ni nani ataiwakilisha Urusi kwenye mazishi hayo.

Papa Francis alifariki Jumatatu kutokana na mshtuko wa moyo ikiwa ni chini ya mwezi mmoja tangu aliporuhusiwa kutoka hospitali alikolazwa kwa wiki wiki tano akiugua homa ya mapafu. Mazishi yake Jumamosi yanatarajiwa kuvutia umma mkubwa.

Jeneza lake ambalo wakati wa uhai wake aliweka wazi anataka liwe la mbao litawekwa mbele ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Peter ndani ya Vatican kisha litapelekwa ndani ya kanisa na baada ya hapo Papa atapelekwa kwenda kupumzishwa kwenye nyumba yake ya milele katika Kanisa la Mtakatifu Maria Mkuu, mjini Roma.