Wakurugenzi wote nchini ambao halmashauri zao zinahitaji kujenga stendi za kisasa wanatakiwa kutenga na kuainisha maeneo ya kujenga stendi hizo na kuanza kutenga fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya kuanza ujenzi wa stendi hizo.
Naibu Waziri-Ofisi ya Rais-Tamisemi, Dk Festo Dugange alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Viti Maalumu, Minza Mjika (CCM) aliyetaka kujua mkakati uliopo wa kujenga stendi katika halmashauri ya Meatu ambayo imeshaandaa eneo la kujenga stendi.
“Wakurugenzi wote nchini, wanatakiwa kuanisha maeneo ya kujenga stendi na kutenga fedha za mapato ya ndani ya halmashauri hizo ili kuanza ujenzi,” alisema.

Kwa halmashauri ambazo hazina uwezo wa kifedha, zimetakiwa kupeleka maombi ofisi ya Rais-Tamisemi kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kuzisaidia kupata fedha.
Kwa upande wake, mbunge wa Makete, Festo Sanga (CCM) alitaka kufahamu ni lini serikali itaanza ujenzi wa stendi ya kisasa ya Makete kupitia miradi ya kimkakati.
Dk Dugange alisema serikali imeendelea kujenga na kuboresha stendi za mabasi katika mamlaka za serikali za mitaa nchini kwa awamu.
Halmashauri ya Wilaya ya Makete inayo stendi yenye eneo la ukubwa wa ekari 3.1 katika eneo la Mabehewani.
Ilielezwa kwamba stendi hiyo inayotumika, iliboreshwa na serikali kupitia mapato ya ndani ya halmashauri na kwamba Sh milioni 40 zilitumika.
Katika mwaka wa fedha 2024/2025, halmashauri imetenga Sh milioni 100 kuiboresha zaidi stendi ya Mabehewani.
Aidha, ili kuwa na stendi kubwa na ya kisasa zaidi, halmashauri ya Makete imetenga eneo la ekari 24.5 na sehemu ya eneo hilo itatengwa kwa ajili ya ujenzi wa stendi ya kisasa.