Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja amefunga Mkutano wa Kundi la Majadiliano la Afrika (AGN) leo tarehe 30 Aprili 2025 katika Ukumbi wa Hotel Verde Mtoni, Zanzibar.
Mkutano huo uliofanyika kwa siku tatu, umewakutanisha washiriki kutoka nchi 54 barani Afrika ambao pamoja na masuala mbalimbali wamejadili ushirikiano katika uhifadhi wa mazingira.

Akizungumza na washiriki wa mkutano huo, Mhandisi Luhemeja amesema kuna umuhimu wa kuwa na Umoja wa Afrika wenye sauti moja yenye nguvu kuhusu mazungumzo ya mabadiliko ya tabianchi.
Amesema Afrika iliyounganishwa yenye sauti dhabiti na ya kijasiri itatoa nafasi kubwa ya kuwasilisha vipaumbele vyake kwenye mikutano ya kimataifa.
“Afrika inahitaji kwenda mbali zaidi juu ya mabadiliko ya hali ya hewa, na kwa hivyo, tunapaswa kwenda pamoja kukabiliana na changamoto hiyo,” amesema.

Amesema Afrika sio bara masikini, hivyo ipo haja ya kuwa na sera na mikakati inayolinda utajiri wa Afrika kwa maendeleo endelevu ya bara hilo.
Pia, Katibu Mkuu amesema kwa kuwa Afrika ndiyo iliyoathiriwa zaidi, kipaumbele cha bara ni kuwa na fedha za uhakika zenye kwa kuzingatia vipaumbele na maslahi.
Amesisitiza mfumo wa ruzuku ni muhimu ili kufadhili miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, hivyo Afrika lazima ihamasishe upatikanaji wa Dola za Marekani Trilioni 1.3 kufikia mwaka 2025.
Mkutano huo ulifunguliwa tarehe 28 Aprili 2025 na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango.



