Balozi za Kanada, Ujerumani, Uholanzi, Norway, Uingereza, Marekani na Umoja wa Ulaya zimesema hali ya kisiasa na usalama ya Sudan Kusini “inazidi kuwa mbaya” tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo
Katika taarifa ya pamoja, balozi hizo zimethibitisha kuwa “zinakubaliana kwa sauti moja” na ripoti iliyotolewa hivi majuzi na Mwenyekiti wa Tume ya Pamoja ya Ufuatiliaji na Tathmini (RJMEC), chombo kinachosimamia utekelezaji wa makubaliano ya amani.
Katika Ripoti yake ya robo mwaka mwenyekiti huyo wa RJMEC Balozi, Jenerali George Owinow alibainisha ” jinsi hali ya kisiasa na usalama ya nchini Sudan Kusini inavyozidi kuzorota siku hadi siku kwa kulinganisha na hali ilivyokuwa mnamo mwaka 2018.
Ripoti hiyo ya robo mwaka ya Tume ya RJMEC imeelezea matukio mabaya ambayo hayajawahi kushuhudiwa tangu kutiwa saini kwa makubaliano ya amani, R-ARCSS zaidi ya miaka sita iliyopita. Matukio hayo ni pamoja na kuingia dosari kwa makubaliano ya amani, migogoro inayohusisha matumizi ya silaha na ghasia, ambayo imezuka kote nchini Sudan Kusini huku wanasiasa wa upinzani wakizuiliwa na kiongozi wao Riek Machar akiwa katika kifungo cha nyumbani.
