📌Wapongeza mifumo ya nishati safi ya kupikia
📌REA yapongezwa kwa kuhamashisha matumizi ya nishati safi
Wajumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) wamefanya ziara ya kutembelea Gereza Kuu la Butimba lililopo jijini Mwanza kwa lengo la kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa mifumo ya nishati safi ya kupikia katika taasisi hiyo.
Ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan linalozitaka taasisi zote zinazotoa huduma kwa watu zaidi ya 100 kuhakikisha zinatumia nishati safi na salama ya kupikia ili kulinda afya za watumiaji na mazingira kwa ujumla.

Akizungumza mara baada ya kukagua utekelezaji wa agizo hilo, Mjumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini, Bw. Florian Haule, amesema kuwa REB imeridhishwa na hatua ambazo tayari zimechukuliwa na uongozi wa gereza hilo katika kuanza kutumia nishati safi ya kupikia, ikiwa ni ishara ya utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kuimarisha matumizi ya nishati mbadala katika taasisi za umma.
“Pamoja na kwamba REA na Jeshi la Magereza tumeingia makubaliano rasmi ya ushirikiano, tumeshuhudia kuwa gereza la Butimba lilikuwa tayari limeanza juhudi hizi kabla ya kuingizwa rasmi katika mpango huu. Hata hivyo, bado kuna changamoto ya uwezo mdogo wa kuhudumia idadi kubwa ya watu waliopo hapa, hivyo tutaongeza nguvu kuhakikisha wanapata huduma bora inayokidhi viwango vinavyotakiwa,” amesema Bw. Haule.
Vilevile, Bodi ya Nishati Vijijini wameshuhudia jeshi la magereza wakipika chakula kwa kutumia gesi ya kupikia (LPG) pamoja na kutumia mkaa mbadala.

Kwa upande wake, Mkuu wa Gereza la Butimba, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP), Masanja Maharangata, ameishukuru Bodi ya Nishati Vijijini pamoja na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kuanzisha mradi huo.
ACP Masanja ameeleza kuwa mfumo huo umeleta mabadiliko makubwa kwa magereza nchini, hususan katika kupunguza gharama za kuni pamoja na changamoto za upatikanaji wake.

Ziara hiyo imeonesha utayari wa Serikali kupitia REA kushirikiana na taasisi za umma kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi na endelevu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kitaifa za kutunza mazingira, kulinda afya na kuimarisha ustawi wa jamii.
Awali Bodi ya Nishati Vijijini imekutana na kufanya mazungumzo na mkandarasi Ceylex wanaosambaza umeme katika mkoa wa Mwanza ambapo wametakiwa kumaliza mradi kwa wakati.


