Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Songea mjini Mwinyi Msolomi amewaasa waandishi wa habari kuzingatia maadili ya taaluma yao kwa kuandika habari zenye weredi na usahihi katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Msolomi ameyasema hayo jana kwenye hafla ya kukabidhi ofisi mpya ya kisasa ya CCM iliyojengwa na mdau wa maendeleo kutoka nchini Canada Amandus Tembo katika Kata ya Bombambali Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.

Alisema waandishi wa habari wanapaswa kuepuka upendeleo, uchochezi na taarifa za upotoshaji ambazo zinaweza kuathiri amani na mshikamano ndani ya Jamii.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa Oddo Mwisho akikata utepe kwenye ofisi mpya ya CCM Kata ya Bombambali.

Alisisitiza kuwa habari zenye upendeleo au uchochezi zinaweza kuhatarisha amani hivyo waandishi wanatakiwa kuhabarisha umma kwa uwazi na ukweli, bila kuegemea upande wowote wa kisiasa.

Waandishi wa habari wana nafasi muhimu ya kusaidia jamii kuelewa sera na mwelekeo wa wagombea na wawe daraja la haki na si chombo cha mashambulizi.

Kwa upande wake mdau wa Maendeleo Amandus Tembo maarufu kwa jina la Toronto alisema kuwa Ujenzi wa ofisi ya Chama kata ya Bombambali ni mwendelezo wa mpango mkakati wake wa kujenga ofisi za CCM Kata zote 21 za Jimbo la Songea mjini ambapo hadi sasa amejenga kwenye kata mbili ya Subira na Bombambili na kugharimu kiasi cha sh. Milioni 60.

Naye mwenyekiti wa CCM Mkoa Oddo Mwisho ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye afla ya kukabidhiwa ofisi hiyo amempongeza Tembo kwa ujenzi wa ofisi za chama za kisasa ambazo atakuwa ameacha alama kubwa lakini amewataka wanachama wa CCM kutunza ofisi hizo ambazo Tembo amejitolea kujenga kwa fedha zake.

Nao wanachama wa CCM Kata ya Bombambali wamemshukuru na kumpongeza mdau huyo wa Maendeleo Tembo kwa kuwajengea ofisi ya kisasa kwani ofisi yao ya mwanzo ilikuwa imechoka sana na wameahidi kuitunza ofisi hiyo kwa gharama kubwa.