MAKUBALIANO kati ya Urusi na Ukraine yameendelea kushuhudiwa kutwa nzima jana Jumatatu na usiku wa kuamkia leo huku kila upande ukionesha ubavu kwa kushambulia ndani ya ardhi ya mwingine.

Urusi iliishambulia mikoa miwili ya mashariki mwa Ukraine ikiwemo Sumy na kuwaua watu watatu. Hayo yalitangazwa na utawala mjini Kyiv.

Urusi nayo kupitia viongozi wake imesema mashambulizi ya Ukraine yamewaua watu watatu katika mkoa wake wa mpakani wa Kursk.

Inaarifiwa vikosi vya Ukraine vilifyetua makombora kuulenga mkoa huo na kisha wanajeshi wake kuingia kwenye ardhi hiyo ya Urusi kwa kutumia magari ya kivita katika eneo lililotegwa mabomu.

Maafisa wa Ukraine hawajazungumzia chochote juu ya madai ya vikosi vyake kuushambulia mkoa huo wa Kursk. Taarifa hizo lakini yumkini zitawastua wengi ndani ya Urusi.

Ukraine ilifanikiwa mwaka jana kukamata sehemu kubwa ya ardhi ya Urusi kwenye mkoa huo wa Kursk lakini Moscow ilitangaza mwezi Aprili kuwa imeikomboa ardhi hiyo.