Pakistan imefanya jaribio la pili la kombora la masafa marefu huku Iran ikimtuma waziri wake wa mambo ya nje kujaribu kuyapatanisha mataifa hayo mawili yenye silaha za nyuklia.
Taarifa ya Pakistan iliyotolewa hivi leo imeeleza kuwa jeshi la nchi hiyo limefanya jaribio la kombora lenye uwezo wa kusafiri umbali wa kilomita 120. Hilo ni jaribio la pili katika muda wa siku mbili. India inaishutumu Pakistan kwa kuhusika na shambulio baya dhidi ya watalii katika eneo lake la Pahalgam huko Kashmir, tuhuma ambazo zimekuwa zikikanushwa na serikali ya Islamabad na kutaka uchunguzi huru ufanyike.
Pakistan imelisifu jeshi lake kwamba liko imara na kusisitiza kuwa majaribio hayo yanalenga kuhakikisha kuwa wanajeshi wako tayari na kuthibitisha iwapo vigezo muhimu vya kiufundi vimekamilika na kwamba silaha hizo zinaweza kutumiwa kwa usahihi. Siku ya Jumamosi,Jeshi la Pakistan lilisema lilifanya jaribio ya kombora lenye uwezo wa kusafiri kilomita 450 bila hata hivyo kutoa maelezo zaidi. Mzozo kati ya India na Pakistan unaendelea kufukuta baada ya shambulizi la mwezi uliopita katika eneo linalozozaniwa la Kashmir.
Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif amesema katika taarifa kuwa ameridhishwa na “maandalizi kamili ya jeshi kwa ulinzi wa taifa, akisisitiza kuwa kufanikiwa kwa majaribio hayo kunaonyesha wazi kwamba ulinzi wa Pakistan uko kwenye mikono salama.” Sharif ameahirisha ziara yake iliyopangwa kufanyika Ijumaa nchini Malaysia kutokana na kuongezeka kwa hali ya wasiwasi kufuatia mvutano huo.
Muhammad Luqman ni mkazi wa Kashmir upande wa Pakistan na amerejelea kauli ya Waziri Mkuu: “Hatuna wasiwasi wowote. Tunajihisi tuko salama kama tulivyokuwa kabla ya mivutano hii. Sababu ni kwamba tunaamini ulinzi wa nchi yetu uko kwenye mikono salama. Kwa hivyo hatuna hofu ya aina yoyote.”
