Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amemkabidhi Mwandishi Bora wa Sekta ya Madini, Dotto Dosca, wa Malunde Blog, Leseni ya Utafiti wa Madini yenye ukubwa wa kilomita za mraba 20 katika hafla ya Tuzo za Samia Kalamu Awards zilizofanyika Mei 05, 2025 jijini Dar es Salaam, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiwa mgeni rasmi wa tuzo hizo.

Mbali na Leseni ya Utafiti, Waziri Mavunde pia amemkabidhi Dotto Dosca zawadi ya fedha taslimu Shilingi Milioni Tano na zawadi ya mapambo ya mezani yaliyotengenezwa kwa madini ya Ruby na Zoisite au Anyolite ambalo ni Jiwe la thamani linachanganya nguvu za moto za Ruby na sifa za utulivu ambapo madini ya Ruby yanajulikana kwa kuleta furaha, shukrani, nguvu ya mwili, na ukuaji.

Zawadi hiyo pia inajumuisha mchanganyiko wa madini ya Amethyst, jiwe la rangi ya zambarau lenye historia ndefu na maana nyingi za kisimba. Amethyst mara nyingi huhusishwa na amani, hekima, na ukuaji wa kiroho.

Aidha, zawadi hiyo ina madini ya Travertine, aina ya jiwe la chokaa linalotokana na mchango wa madini kutoka kwenye chemchemi za maji ya moto au baridi, pamoja na madini ya Fedha, metali ya thamani yenye rangi ya kung’aa inayotumika kutengeneza mapambo, sarafu, na vifaa mbalimbali.

Zawadi hiyo ya kipekee imeandaliwa na Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC), kilichopo jijini Arusha, ambacho kinatoa mafunzo ya uongezaji thamani ya madini ya vito.

Tuzo za Samia Kalamu ni juhudi za kuhamasisha na kukuza uandishi na uchapishaji wa maudhui ya ndani, hasa katika vyombo vya habari, kwa lengo la kuchochea utafiti na uchambuzi kuhusu maendeleo ya nchi, uwajibikaji, uzalendo, na kujenga taswira chanya ya taifa.

Katika hafla hiyo, Waziri Mavunde ameongozana na Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Eng. Yahya Samamba.

Tuzo hizo za Samia Kalamu Awards zimeandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).