Mpango wa upande mmoja wa kusitisha mapigano uliotangazwa na Moscow umeanza kutekelezwa muda mfupi baada ya saa sita usiku.

Usitishaji huo wa mapigano kwa saa 72 unatarajiwa kudumu hadi saa sita usiku Jumamosi kuamkia Jumapili. Rais wa Urusi Vladmir Putin alitangaza usitishaji huo kwenda sambamba na maadhimisho ya kila mwaka ya Urusi ya Siku ya Ushindi mnamo Mei 9 ambayo ni kumbukumbu ya kumazilika kwa Vita vya Pili Vikuu vya Dunia.

Hata hivyo, Ukraine imepuuzilia mbali hatua hiyo ya Urusi ikisema ni ya kiishara tu na inaendelea kushinikiza, pamoja na Marekani, usitishaji mapigano wa angalau siku 30. Rais Volodymyr Zelensky amesema katika hotuba yake ya usiku kuwa hawataliondoa pendekezo lao hilo, kwa sababu linatoa fursa ya kweli ya suluhisho la kidiplomasia.

Viongozi wa kigeniakiwemo Rais Xi Jinping wa China, Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil na Aleksandar Vucic wa Serbia wako Moscow kuhudhuria maadhimisho hayo.