Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) zimesaini hati ya makubaliano inayolenga kuboresha na kuimarisha miundombinu ya usafirishaji, ikiwemo bandari sambamba kuchochea shughuli za kiuchumi wa nchi hizo.
Makubaliano haya ni sehemu ya jitihada za pamoja za kukuza biashara ya mipakani, hususan kupitia Ziwa Tanganyika, ambapo Tanzania inaendelea na ujenzi wa bandari ya Karema mkoani Katavi pamoja na maboresho ya bandari ya Kigoma.
Akijibu swali la Mbunge wa Momba, Mheshimiwa Condester Michael Sichalwe, kuhusu hatua za Serikali katika kuhakikisha Tanzania inanufaika na soko la DRC licha ya nchi hiyo kutoanza ujenzi wa bandari upande wake, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Bw David Kihenzile, alifafanua kuwa Serikali imejipanga kikamilifu kushirikiana na DRC kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ili kufungua fursa za kiuchumi baina ya nchi hizo mbili kupitia sekta ya usafirishaji ikiwemo bandari.
“Serikali kupitia TPA imeanza uboreshaji wa bandari ya Kigoma pamoja na ujenzi wa bandari mpya ya Karema kwa lengo la kushirikiana na DRC katika kukuza biashara kupitia Ziwa Tanganyika,” alisema Bw. Kihenzile.
Aidha, alieleza kuwa tayari TPA inaendelea na upembuzi yakinifu na usanifu wa awali kwa ajili ya kuendeleza bandari ya Moba upande wa DRC, huku ujenzi wa bandari ya Karema ukiendelea kwa ushirikiano na mwekezaji binafsi.
Katika mjadala huo, Mheshimiwa Sichalwe aliitaka Serikali kuchukua hatua zaidi kwa kuhakikisha kunakuwa na barabara ya moja kwa moja kutoka bandari ya Moba hadi Lubumbashi nchini DRC, ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kuepuka usumbufu wa kupitia Zambia.
“Mheshimiwa Naibu Waziri, ulipokutana na meneja wa TPA, alisisitiza umuhimu wa barabara ya Moba hadi Lubumbashi. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha ujenzi wa barabara hiyo unaanza?” alihoji Mheshimiwa Sichalwe.
Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri Kihenzile alikiri kuwa barabara hiyo ni ya kimkakati na Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa miundombinu ya kuunganisha masoko ya DRC, hususan Lubumbashi, inaboreshwa.
Aliongeza kuwa Tanzania ina fursa ya kipekee ya kuhudumia nchi zisizo na bandari kama Zambia na DRC, ambapo kwa sasa Zambia hupitisha zaidi ya tani milioni 7 za mizigo kupitia Tanzania, huku DRC ikifikia zaidi ya tani milioni 10.
“Tunaendelea kuwekeza katika bandari zetu za mikoa ya Ziwa Tanganyika ili kufungua fursa zaidi kwa wafanyabiashara wetu,” alihitimisha Naibu Waziri.
