Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mwanza

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema Serikali ipo kwenye mchakato wa mwisho wa kununua mitambo mitatu ya kisasa kwa ajili ya kushughulikia changamoto ya magugu maji katika Ziwa Victoria.

Mhe. Mtanda amesema mitambo hiyo itatumika kusafishia gugu maji ambalo limekuwa changamoto kubwa katika Ziwa Victoria, lakini tayari Serikali imechukua hatua kwa kuyaondoa na muda sio mrefu changamoto hiyo itakuwa imetatuliwa kwa asilimia kubwa. 

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mha. Cyprian Luhemeja akielezea jambo kwa baadhi ya viongozi aliofuatana nao katika ukaguzi wa zoezi la utoaji wa Gugu maji linaloendelea Ziwa Victoria ambapo hadi Mei 10, 2025 zaidi ya tani 600 zimeondolewa.

Ameyasema hayo wakati wa ziara ya ukaguzi wa zoezi la udhibiti wa magugu maji Mei 10, 2025 ambapo amesema wanamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kusikia kilio cha wananchi wa Jiji la Mwanza kuhusu changamoto hiyo.

“Hapa tuna Feri tatu lakini baada ya ujio wa magugu maji hasa yale madogo madogo ambayo tayari tumeanza kuyavuna yalikuwa yakikwamisha feri zetu na sasa tunatumia Shilingi 2 milioni kwa siku kwa ajili ya usafi.”

“Msitu unaoonekana ndani ya ziwa ni athari zenyewe za magugu maji na kufanya kukwamisha kazi zetu za kila siku tunazofanya hivyo habari njema ni kwamba Rais Samia amesikia kilio chetu,” amesema Mhe. Mtanda.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda (kulia) akielezea jambo kwa baadhi ya viongozi aliotanguzana nao katika ukaguzi wa zoezi la utoaji wa Gugu maji linaloendelea Ziwa Victoria ambapo hadi Mei 10, 2025 zaidi ya tani 600 zimeondolewa. Wengine katika picha ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mha. Cyprian Luhemeja na Meneja wa NEMC Kanda ya Ziwa Bw. Jerome Kayombo.

Kwa upande wa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mha. Cyprian Lehemeja amesema magugu maji yanaleta athari kubwa ya mazingira, uchumi na kijamii ikiwemo kuathiri viumbe hai vinavyoishi kwenye maji.

“Kuna magugu maji ya aina mbili kuna yale mapya ambayo wenzetu wa Bonde la Maji na kikosi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wanayafanyia kazi na hadi sasa hali yake kidogo inaridhisha japo bado ziwa halipo safi.

“Changamoto kubwa ni magugu yale ya zamani ambayo yanahitaji nguvu ya ziada na tayari tumeanza zoezi la kukabiliana nayo kwa kuyakata ili kuona spidi ya kukua yanapungua na hatua ya pili ni kununua mashine ya kisasa kama ambavyo ilivyoelekezwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa,” anasema Mha. Luhemeja. 

Ameongeza kuwa changamoto bado ipo sababu yanakuwa kwa haraka lakini kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa changamoto hiyo itadhibitiwa na malalamiko yaliyokuwepo tayari yameondoka na Ofisi ya Makamu wa Rais inajitahidi kukabiliana na changamoto ya mazingira.

Meneja wa NEMC Kanda ya Ziwa Bw. Jerome Kayombo (mwenye fulana nyeupe) akifafanya jambo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda (katikati) pamoja na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mha. Cyprian Luhemeja wakati wakikagua zoezi la uondoaji gugu maji katika Ziwa Victoria, Mei 10, 2025.

“Kikubwa tunaendelea kuweka usafi na kufanya ziwa linakuwa salama na kuendelea na matumizi kama awali na wananchi wataendelea na shughuli zao bila changamoto yoyote.”

Hadi Mei 10, 2025 zaidi ya tani 600 ya gugu maji yametolewa katika Ziwa Victoria huku zoezi hilo likiwa endelevu kwa ajili ya kukabiliana na changamoto hiyo ya Uhifadhi na Utunzaji wa Mazingira.

Mkuu wa Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza Mhe. Johari Samizi akifafanua jambo kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mha. Cyprian Luhemeja wakati wa zoezi la utoaji wa Gugu maji linaloendelea katika Ziwa Victoria, Mei 10, 2025.
 
. Baadhi ya vibarua wakiwa katika zoezi la utoaji gugu maji ndani ya Ziwa Victoria Mei 10, 2025 ambapo zaidi ya tani 600 tayari zimeondolewa katika zoezi linaloendelea la utoaji gugu maji.PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS