Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Serikali kupitia wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum imeendelea kuimarisha mifumo ya kisheria kwa kufanya marekebisho ya Sheria Tatu ambazo ni Sheria ya Mtoto, Sura ya 13, Sheria ya Makosa ya Kimtandao, Sura ya 443, na Sheria ya Msaada wa Kisheria, Sura ya 21.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu siku ya familia ambayo hufanyika Mei 15 ya kila mwaka Waziri wa Wizara hiyo Dkt.Dorothy Gwajima alisema marekebisho hayo yamelenga kuondoa upungufu unaojitokeza katika utekelezaji wa masharti katika sheria husika ili kuimarisha ulinzi na maslahi bora ya mtoto.
Aidha alisema, kupitia marekebisho hayo adhabu dhidi ya vitendo vya ukatili mtandaoni zimeainishwa katika kifungu cha 13 (3) na (4) ya Sheria ya Makosa ya Kimtandao Sura ya 443.
“Katika utekelezaji wa sheria hiyo atakaebainika kushiriki vitendo vya ukatili mtandaoni atakabiliwa na adhabu ya faini isiyopungua shilingi millioni 50 au thamani mara tatu ya faida aliyoipata kupitia kitendo hicho au kifungo kisichopungua miaka 7 au vyote kwa pamoja .
Aidha alisema,vile vile inaweza kutolewa adhabu nyingine itakayoamriwa na mahakama ikiwemo kulipa fidia ya kiasi kitakachoamriwa na mahakama kwa manusura wa ukatili wa kimtandao.

Kuhusu vitendo vya ukeketaji alisema,katika kukabiliana na vitendo vitendo hivyo, kifungu maalum cha 158A cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 kinatoa adhabu kwa makosa ya ukeketaji.
Alisema, atakayebainika kushiriki vitendo vya ukeketaji atakabiliwa na adhabu ya faini isiyopungua shilingi milioni 2 au kifungo kisichopungua miaka 5 na kisichozidi miaka 15 au vyote kwa pamoja au kulipa fidia ya kiasi kitakachoamriwa na Mahakama kwa yule aliyetendewa kosa hilo.
“Aidha, Wizara inaendelea kuwakumbusha Wazazi au Walezi kuhusu takwa la kisheria katika Sheria ya Mtoto Sura ya 13 kifungu cha 7 la ulazima wa kutoa malezi na matunzo kwa Watoto.
Alisema, mzazi au mlezi asipotimiza wajibu wake anakabiliwa na adhabu ya faini isiyozidi shilingi Milioni 5 au kifungo cha miezi 6 au vyote kwa pamoja.
Aidha ameshaurimikoa na halmashauri kuadhimisha siku hii kwa kuandaa afua za kuelimisha na kuchochea mijadala katika Jamii kwa kutumia wataalamu wa malezi chanya ya watoto na familia ikiwa pamoja na viongozi wa Dini ili kutafuta ufumbuzi wa migogoro katika familia na malezi duni ya watoto.
Aidha alisema, mijadala hiyo ilenge namna bora zaidi ya kushughulikia changamoto za watoto wanaokimbia familia zao na kuja kuishi na kufanya kazi mitaani sambamba na mmomonyoko wa maadili tunaoushuhudia katika jamii.
“ Niwaombe Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa kupitia Watendaji ngazi za Halmashauri wataratibu na kuandaa mijadala ili kukabiliana na changamoto za malezi ya watoto ambazo nyingi zinatokana na matokeo hasi ya maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano, mwingiliano wa mila na desturi zisizofaa za mataifa mengine na migogoro ya wenza au wanandao katika familia.