Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu), William Lukuvi, amethibitisha kuwa maandalizi ya mazishi ya Hayati Cleopa David Msuya, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu wa Tanzania, yamekamilika.
Waziri Lukuvi alitoa taarifa hiyo leo tarehe 11 Mei 2025 akiwa ziarani wilayani Mwanga, Mkoani Kilimanjaro, alipotembelea maeneo ambayo mwili wa Hayati Msuya unatarajiwa kupita katika safari yake ya mwisho.

Waziri Lukuvi, akiwa ameambatana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mhe. Hamza Juma, pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdini Babu, alikagua maeneo ambayo mwili wa Hayati Cleopa David Msuya unatarajiwa kupita kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho.
Waziri Lukuvi alieleza kuwa ziara yao ilikuwa ni kuhakikisha kuwa maandalizi yote ya safari ya mwisho ya Mzee Msuya yanakamilika kwa heshima hali ya juu.
Waziri Lukuvi alisisitiza kuwa, “Tumekuja kushuhudia na kusimamia ili kuhakikisha safari ya mwisho ya Hayati Cleopa David Msuya inakamilika kwa heshima zote.”
Aidha, Waziri Lukuvi alitoa shukrani kwa wananchi wa Kilimanjaro, akisema kuwa wamefanya kazi kubwa kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdini Babu, kuhakikisha kwamba mwili wa mzee Msuya utaagwa kwa heshima katika Wilaya ya Mwanga kabla ya kuelekea Usangi.

“Mwili utaagwa Mwanga Mjini na baadaye utapanda Usangi ili wananchi wa Usangi wapate nafasi ya kutoa heshima zao za mwisho,” aliongeza.
Wakati akizungumzia mchakato wa mazishi, Waziri Lukuvi alisema kwamba keshokutwa kutakuwa na ibada maalumu, na baada ya ibada hiyo, mazishi ya Hayati Cleopa David Msuya yatafanyika nyumbani kwake.
Alitoa wito kwa wananchi wa Wilaya ya Mwanga na Kilimanjaro kwa ujumla kushirikiana katika kipindi hiki cha maombolezo, ili kudumisha umoja wa kitaifa katika kumuheshimu mzee Msuya, ambaye ameleta mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa.



