Na Mwandishi Wetu, JamhiriMedia, Dar es Salaam

KATIKA jitihada za kuendana na mtaala mpya wa elimu uliozinduliwa hivi karibuni na Serikali, unaojumuisha Mahili 11 yanayolenga kuendeleza ujuzi na stadi kwa wanafunzi, shule za Tusiime zimechagua program za Kompyuta kama kipaumbele chao.

“Tukiwa na dira ya kuandaa wanafunzi kwa maisha ya kesho yanayotawaliwa na teknolojia, hususan katika zama hizi za akili mnemba Artificial Intelligence (AI), shule zetu za Tusiime kuanzia shule ya awali, msingi na sekondari mpaka kidato cha sita zimeanza rasmi utekelezaji wa somo la Introduction to Complete Programming kwa wanafunzi wa ngazi mbalimbali,” amesema leo Mkurugenzi wa shule hizo, Dk Albert Katagira.

Alisema lengo la kuanza kufundisha program za kompyuta ni kuhakikisha kuwa wakifika kidato cha sita, kila mwanafunzi wa Tusiime awe na ujuzi mpana wa kujua program mbalimbaali za kompyuta.

Dk Katagira alisema mafunzo hayo yatamwezesha mwanafunzi kujiajiri kupitia utengenezaji wa programu rahisi, kuunda vikundi vya programmer rika (peer programming groups), kushiriki kwenye miradi ya pamoja ya teknolojia na kutengeneza suluhisho za kidigitali kwa changamoto za kijamii na kiuchumi.

“Kwa sasa, mafunzo ya awali yameshaanza kwa vitendo, ambapo wanafunzi wetu wa shule ya msingi tayari wanafundishwa msingi wa programming, ikiwemo kutumia lugha kama Scratch na Python (kwa baadaye),” amesema na kuongeza.

“Kwa kutambua umuhimu wa ushirikiano na jamii, hususan wazazi, shule za Tusiime inatekeleza kampeni ya uhamasishaji ili kutoa uelewa kwa wazazi kuhusu faida za mahili ya Programming,” amesema

Aidha amesema shule hizo zinatoa nafasi kwa wadau mbalimbali kushirikiana nao katika safari hii ya mapinduzi ya elimu, kuandaa wanafunzi wanaoweza kuhimili ushindani wa soko la ajira la kidigitali.

“Tunawaalika wazazi, wadau wa elimu na jamii kwa ujumla kuunga mkono juhudi hizi katika kuwajengea vijana wetu msingi imara wa mafanikio ya baadaye kwasababu shule za Tusiime tunajenga kizazi cha kesho chenye maarifa, ujuzi na ubunifu,” amesema Dk Katagira.