Na Kija Elias, JamhuriMedia, Mwanga
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Alex Malasusa, amemzungumzia hayati Cleopa Msuya kama mzee wa hekima, busara, na upendo, ambaye alijitahidi kuwa na amani na watu wote.
Dk. Malasusa alisema hayo wakati wa mahubiri yake katika ibada ya mazishi ya mzee Msuya, yaliyofanyika katika Kanisa la KKKT Usangi.
Akizungumza mbele ya waombolezaji, Dk. Malasusa alisema kuwa watu wengi walimuheshimu hayati Msuya si kwa sababu ya nguvu au mamlaka yake aliyokuwa nayo, bali kwa sababu ya hekima, busara, na jinsi alivyokuwa na mapenzi kwa watu.
Alieleza kuwa, hayati Msuya alijitahidi kila wakati kutafuta amani, jambo lililowafanya wengi kumheshimu na kumuenzi.
“Hayati Msuya alikuwa mzee wa kuchota hekima na busara, watu walimuheshimu, sote tulimuheshimu si kwamba alikuwa na nguvu sana, bali kwa sababu ya hekima yake na busara yake, si kwa sababu alitisha, lakini kwa sababu alitanguliza sana kutafuta amani na watu wote,” alisema Dk. Malasusa.
Aidha, Dk. Malasusa alisisitiza kwamba wanadamu wanapojua kuwa maisha yao ni ya kuhesabika, wanapaswa kuishi kwa kumpendeza Mungu na kwa kutafuta amani na watu wote, huku akinukuu mstari kutoka katika Kitabu cha Waebrania 12:14, akisema:
“Tafuteni kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao.”
Akielezea maisha ya hayati Msuya, Dk. Malasusa alisema kuwa Msuya alitafuta sana kuwa na amani na watu wote, na kwamba miongoni mwa watumishi wa serikali waliokuwa wakifanya kazi na yeye walielezea juhudi zake katika kuleta maelewano.
“Baba huyu aliyelala umauti ni baba ambaye alitafuta sana kuwa na amani na watu wote, najua miongoni mwa watumishi wa serikali waliokuwa very serious ni huyu baba, wale waliofanya kazi naye walikuwa wakituhadithia,” alieleza Askofu Malasusa.
Hayati Cleopa Msuya alikuwa mzee mwenye mchango mkubwa katika siasa za Tanzania, na alihudumu katika nyadhifa mbalimbali za juu serikalini, ikiwa ni pamoja na wadhifa wa Waziri Mkuu, alikuwa na heshima kubwa kwa wengi kutokana na tabia yake ya kutafuta umoja, amani, na ustawi wa jamii.
Msuya alifariki dunia Jumatano ya Mei 7,2025 Kijitonyama Jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya moyo.
Viongozi mbalimbali wa chama na serikali walishiriki ibada hiyo akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar Hussein Ali Mwinyi, Makamu wa Rais Philip Mpango, Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete, Spika wa Bunge Tulia Akson.