Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameongoza waombolezaji katika ibada ya kuuaga mwili wa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu, Hayati Cleopa David Msuya, iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Usangi Kivindu, na kufuatiwa na mazishi nyumbani kwa marehemu, kijiji cha Chomvu, wilaya ya Mwanga, mkoa wa Kilimanjaro.
Taarifa iliyotolewa na Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Bw. Shaaban Kissu imesema Rais Dkt. Samia ameeleza kwa masikitiko makubwa kumpoteza kiongozi ambaye sio tu aliitumikia Tanzania kwa uadilifu wa hali ya juu, bali pia aliweka msingi imara wa maendeleo ya Taifa katika nyanja za siasa, uchumi na jamii kwa miongo kadhaa.
“Tumshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha ya Baba yetu, Mzee Cleopa David Msuya
Bila shaka, mtakubaliana nami kwamba Mzee huyu amekuwa zawadi siyo tu kwa familia na jamii yake, bali kwa taifa zima,” alisema Rais Dkt. Samia.

Akitoa salamu za pole kwa familia, ndugu na watanzania kwa ujumla, Rais Dkt. Samia amesema Hayati Msuya alikuwa kiongozi mwadilifu, mchapakazi, na mzalendo aliyetoa maisha yake yote kwa ajili ya kuwatumikia watanzania, pamoja na kuwa mfano wa kipekee katika historia ya uongozi tangu mwaka 1956 alipoajiriwa kama Afisa Maendeleo ya Jamii, hadi mwaka 2000 alipostaafu siasa na utumishi wa umma.
Akiwa Waziri wa Fedha kwa vipindi tofauti (mwaka 1972 – 1975, mwaka 1983 – 1985, na mwaka 1985 – 1990), Hayati Msuya alihusika kwa kiasi kikubwa katika kutafuta fedha za maendeleo na hata kusaidia harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika, ikiwemo kushiriki kutafuta fedha za ujenzi wa miundombinu ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).
Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Samia amesema Hayati Cleopa Msuya alikuwa kiongozi aliyehamasisha matumizi ya utaalamu katika utawala na maamuzi ya kisera, huku akisisitiza uadilifu na matumizi bora ya rasilimali za Taifa.

“Aliamini kuwa ujuzi na utaalamu una nafasi kubwa katika kuleta maendeleo.
Alitufundisha kuwa kiongozi bora ni yule anayesikiliza wataalamu na kuchukua maamuzi ya busara,” aliongeza Rais Dkt. Samia.
Hata baada ya kustaafu, Hayati Msuya aliendelea kutoa ushauri muhimu kwa viongozi wa sasa serikalini, akibaki kuwa sauti ya busara na hekima katika masuala ya maendeleo ya Taifa.
Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa aliwahi kumtembelea mara kadhaa kwa lengo la kupata maoni na ushauri wake kuhusu masuala mbalimbali ya kiaifa.
Aidha, Rais Dkt. Samia ameongeza kuwa Taifa litaendelea kumuenzi Hayati Cleopa David Msuya kwa kutambua mchango wake mkubwa na kutumia mafunzo ya maisha yake katika kuijenga Tanzania ya leo na kesho.
Hayati Msuya alifariki dunia tarehe 7 Mei, 2025 kwa maradhi ya moyo katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Emillio Mzena, Jijini Dar es Salaam.









