Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo, ameitaka jamii kuzingatia matumizi ya pombe kwa kiasi, hasa pombe kali, kufuatia utafiti uliofanywa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) unaoonesha kuwa unywaji pombe kupindukia miongoni mwa vijana ni changamoto kubwa katika jamii.

Akizungumza Mei 12, 2025, mara baada ya kikao cha pamoja kati ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo na taasisi mbalimbali zikiwemo TBS, Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA), na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Waziri Jafo alisema kuwa serikali imeanza kuchukua hatua baada ya kupewa maelekezo na kamati hiyo kushughulikia tatizo la unywaji pombe uliokithiri.

“Kazi imeenda vizuri, isipokuwa ni jukumu la jamii kuwaelekeza vijana wetu kwamba kila jambo lina mipaka. Hata wanapokwenda kwenye starehe, lazima wawe na kiasi. Jamii lazima ihakikishe inalinda hili kwa pamoja,” alisema Waziri Jafo.

Aidha, Waziri huyo alieleza kuwa wizara yake inalenga kuhakikisha maendeleo ya wananchi yanapatikana kupitia uzalishaji wa bidhaa zenye viwango bora ili kumlinda mlaji.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mariamu Ditopile, alisema kuwa walikuwa na majadiliano mazuri na wizara pamoja na taasisi husika, ambapo wamepata uelewa mpana kuhusu kazi zinazofanywa na taasisi hizo.

“Wajumbe wamepata uelewa kuhusu mifumo ya kutambua bidhaa zinazozalishwa nchini ili kubaini uhalali wake, jambo ambalo litasaidia katika kuongeza makusanyo ya mapato,” alisema Ditopile, ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum.

Mbunge huyo alisisitiza kuwa TBS na WMA zihakikishe waingizaji wa bidhaa nchini wanafuata vigezo vilivyowekwa ili mlaji wa mwisho apate bidhaa salama na zenye ubora.