Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Tangu kuibuka kwa sakata la msanii Ibraah kutaka kujiondoa katika lebo ya Konde Gang, kwa mara ya kwanza Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Lebo hiyo, Rajab Abdul ‘Harmonize’ amerekodi video fupi akieleza vitu vingi ikiwemo kukanusha kumdai Sh bilioni 1 msanii huyo.

Video hiyo inapatikana kwenye ukurasa wa mtandao wa Instagram ya msanii huyo.

“Nikiri kwamba mdogo wangu amenieleza kuwa anataka kujiondoa kwenye ‘label’ na mimi nilimjibu kwa wema kuwa nakutakia kila la kheri. Nilimwelekeza akae na viongozi wa Konde Gang wasome mkataba wake waone namna bora ya kuachana kwa amani,” amesema Harmonize.

Amefafanua kuwa mkataba ulieleza kuwa msanii akitaka kujiondoa huku akimiliki kazi zote alizozifanya chini ya Konde Gang, ikiwemo zile alizoshirikiana naye, inabidi alipe kiasi kilichotajwa miaka minne iliyopita. Hata hivyo, Harmonize amesisitiza kuwa hajawahi kumdai Ibraah kiasi hicho cha fedha.

“Namtakia kila la kheri, kwa sasa yeye ni msanii anayejitegemea. Promoters mkitaka kumpa ‘show’ muiteni, apate riziki aisaidie familia yake,” ameongeza.

Akizungumzia kuhusu tuhuma kuwa alimuita Ibraah chumbani na kumtaka amtoe mama yake, Harmonize alisema, “Inahuzunisha sana. Mtoto akiunyea mkono huwezi kuukata. Nimemuachia Mungu, nimemsamehe, na ninamuombea.”

“Atazungumza na Mungu wake binafsi atapata majibu yeye binafsi kwa alichokifanya kwa upande wangu nimemalizana naye.

Harmonize alihitimisha kwa kusema kuwa hana chuki, hataki pesa imchafue, na hana haja ya kusubiri msamaha kutoka kwa Ibraah bali anamuombea heri katika maisha yake mapya ya kujitegemea.