*Ni kwa kupuuzwa ombi la Mbowe la kuundwa ‘kamati ya maridhiano’
*Makundi ya viongozi, wanachama waandamizi wadai chuki itaua chama
*Wadau wajiuliza iwapo CHAUMMA itaweza kuhimili vishindo
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,Dar es Salaam
Wahenga wanasema sikio la kufa halisikii dawa. Hiyo ndiyo hali inayokikumba Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa sasa.
Chama hicho ambacho kabla ya mpasuko kilikuwa kikitambulika kama chama kikuu cha upinzani nchini, huenda kikazorota iwapo hatua stahiki hazitachukuliwa kuzuia mpasuko na mifarakano ya ndani inayofukuta.
Sasa viongozi waandamizi na wanachama kadhaa wenye ushawishi wameanza kujiengua kupitia kundi maarufu la ‘G55’ linaloonekana waziwazi kutofautiana sera na mitizamo na uongozi wa Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu, bila kujali kuwa kiongozi huyo kwa sasa yupo mahabusu kwa tuhuma za uhaini.
Mwishoni mwa wiki, viongozi wa G55 waliokuwa wajumbe wa Sekretarieti ya Chadema iliyomaliza muda wake, walitangaza kuondoka kwa kile walichokiita; “kuepuka matatizo yaliyoko ndani ya chama.”
Wajumbe hao, wakiongozwa na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Bara, Benson Kigaila, wamesema wanaendelea hatua inayofuata baada ya uamuzi huo.
Wenhgine ni aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, Catherine Ruge na John Mrema.

KAULI ZA VIONGOZI
Aliyekuwa Mweka Hazina Kanda ya Kaskazini, Amanuel Kimambo, anasema inahuzunisha kuona juhudi walizofanya kwa miaka mingi zikiharibiwa ndani ya mudamfupi.
“Hatuwezi kufurahia maamuzi haya, lakini tumejipatia sababu za kujitoa katika chama chetu cha Chadema,” amesema.
Kimambo, aliyewahi kuwaa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (BAVICHA) Mkoa wa Arusha na Katibu wa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema; anawakilisha mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga.
Amedai kuwa kama Mweka Hazina na Mjumbe wa Baraza Kuu, ameshuhudia mabadiliko ya maazimio ambayo sasa yanawaletea matatizo.
“Hatuwezi kusema ‘No Reform, No election’ wakati Baraza lilituelekeza kujiandaa kwa uchaguzi. Tusema tunahitaji mabadiliko, lakini si kususia uchaguzi,” amesema Kimambo.
Amesema kama vijana wenye ndoto, walijadili na kupeleka mapendekezo kwa viongozi wapya wa juu wa chama, lakini walionekana wasaliti na wenye uchu wa madaraka.
“Hali hii imenifanya nijisikie kutothaminiwa ndani ya chama. Nilipokea barua kutoka tawini kwangu ikinitaka nijieleze kwa nini ni mmoja wa kundi la G55, kinyume na katiba.
“Nilimwomba kiongozi wa tawi anipatie nafasi ya kujieleza, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa. Aprili 25, 2025 nilipokea barua nyingine ikinitaka nijieleze kwa nini nilisambaza barua kwenye mitandao ya kijamii. Ikanililetea shida sana.
“Mpaka sasa, tumekumbwa na chuki inayotufanya tuonekane si familia ya Chadema, jambo ambalo mwasisi wa chama, Freeman Mbowe, hakutufunza. Alitufunza upendo, mshikamano na kusaidiana hata katika nyakati ngumu.
“Hata hivyo, tumeingia katika mazingira ya chuki na kutokuelewana, ambapo wiki iliyopita nilipata safari ya kwenda Afrika Kusini, lakini maneno ya uchonganishi yalitolewa, yakisema kuwa mimi ni msaliti,” amesema Kimambo.

Amesema watu wanaofanya fitina hizo ni viongozi ndani ya chama ambao wanajinasibu kuwa wanataka mabadiliko ya kweli.
Kwa bahati mbaya, anasema, kuna dalili kuwa chuki hizo zina baraka ya uongozi wa juu kwa kuwa hata zikiripotiwa hakuna hatua inayochukuliwa.
“Nimeona Chadema sio familia yangu tena, hivyo nimejiunga na G55 kwa sababu tulijitolea kufanya kazi za chama bila malipo, lakini sasa Lema amekuwa mwasisi wa watu kufukuzwa bila sababu,” analalamika mwanachama huyo kijana.
Mwingine aliyeondoka Chadema ni Gimbi Doto Masaba wa Kanda ya Serengeti aliyejiunga mwaka 2010 na kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Wilaya ya Itilima mwaka 2013.
Anasema wakati huo chama kilikuwa kinajiandaa kwa uchaguzi wa serikali za mitaa chini yake na mwaka uliofuata akawa Mbunge wa Viti Maalumu hadi mwaka 2020.
“Katika kipindi hicho, nilichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti (mikoa ya Mara, Simiyu na Shinyanga) chini ya John Heche (sasa Makamu Mwenyekiti Taifa).
“Nikachaguliwa tena (mwaka jana) kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kanda, lakini baada ya kutafakari, nimeona kusimamia ajenda ya ‘No reform, No Election’ haina maana kwa sababu inamnyima mtu haki na fursa ya kuwa mwenyekiti wa kitongoji, diwani, mbunge au Rais.
“Nimetafakari na kugundua kuwa, kama chama hakitokwenda kwenye uchaguzi, ndoto zetu hazitakuwa na maana. Leo, najiondoa ili kulinda heshima yangu, kutokana na chuki kwa kuwa nilikuwa meneja wa kampeni wa Mbowe,” amesema.
Hali ipo hivyo pia kwa aliyekuwa Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema; aliyejiunga na chama mwaka 2004.
“Wananchi wanataka kujua hadithi ya Chadema ina majimbo mangapi na tunashinda kwa mifumo gani. Lakini sasa wanachoshuhudia ni chama kilichokuwa juu, kikiporomoka! Hii inawakatisha tamaa Watanzania.
“Ugonjwa umeingia ndani ya chama chenu Watanzania. Sio wanachama wa Chadema tu, bali hata wa CCM, CUF na watu wasio na chama. Watanzania wanataka kupata matokeo bora kutoka Chadema,” amesema Lema.

Naye amezungumzia chuku ndani ya chama akisema: “Chuki imekuwa kubwa sana! Hivi sasa haiwezekani watu wa magharibi kukutana na mashariki au kusini na magharibi.
“Tunachotaka ni Serikali iwape Watanzania uhuru wa kuwaweka pamoja, kwa sababu ukijihusisha na Lissu sawa; ukienda kwa Mbowe, wewe ni muasi! Tunachokitaka ni Serikali itupe uhuru kwa lazima.”
Kundi jingine
Kundi la pili la viongozi wanaoondoka Chadema ni lile linalohusisha wanachama kutoka kanda za Pwani, Serengeti, Kaskazini, Kusini, Kati, Nyasa, Victoria na Magharibi.
Hawa wametangaza kujivua uanachama kwa sababu mbalimbali zikiwamo kukithiri kwa ukiukwaji wa Katiba ya chama, huku pia chuki na ubaguzi dhidi ya viongozi na makada waliokuwa wakimuunga mkono Mbowe vikitajwa.
Waliotangaza kujivua uanachama na nafasi zao mbali na Kimambo na Lema wa Kilimanjaro, ni Jackson Jingu (Makamu Mwenyekiti Kanda ya Kati) na Esther Fulano (Katibu wa BAWACHA Kanda ya Victoria na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chadema Taifa).
Wengine ni Doris Mpatili (Mwenyekiti Kamati ya Mafunzo Kanda ya Victoria), Hadija Said Mwago (Mjumbe wa Baraza Kuu Chadema kupitia BAWACHA, Mwenyekiti wa BAWACHA Jimbo la Mbagala), Hanifa Chiwili (Katibu wa Kamati ya Maadili Kanda ya Pwani, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Pwani Kusini) na Jackline Kimambo (Katibu wa Kamati ya Mafunzo Kanda ya Kaskazini)
Pia wamo Abuu Mohamed Mrope (Katibu wa Chadema Kanda na Mweka Hazina Kanda ya Kusini), Magreth Mlekwa (Katibu wa BAWACHA Kanda ya Nyasa), Stewart Kaking (Ofisa wa Kanda ya Kusini), John Lema (Ofisa Oganaizesheni, Mafunzo na Uchaguzi)
Lema ndiye mwimbaji wa wimbo maarufu wa “Naapa Naahidi Mbele ya Mungu, Chadema Nitakulinda Mpaka Kufa”.

Ombi la Mbowe
Mara baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa ndani wa Chadema, Januari mwaka huu, mgombea aliyeshindwa nafasi ya Mwenyekiti Taifa, Mbowe, alimwomba Mwenyekiti mpya, Lissu, kuunda kamati ya maridhiano ili kuponya majeraha yaliyotokea wakati wa kampeni.
Mbowe aliamini kwamba kampeni za uchaguzi wa ndani wa Chadema zimeacha majeraha ambayo kama yasipotibiwa, yangesababisha madhara ndani ya chama.
Hata hivyo, si Lissu wala viongozi wengine waandamizi (wapya) walioonyesha nia ya kufanya hivyo.
Hata walipokusatana Bagamoyo kwa wiki kadhaa, suala hilo halikupewa kipaumbele na sasa Chadema imegawanyika kati ya watu wa Lissu na watu wa Mbowe.
Awali, wakati wa kampeni, aliyewahi kuwa Mbunge wa Arusha na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Godbless Lema, alisema kuondoka Chadema kwa mwanachama yeyote huwa ni pigo na pengo lisilozibika.
Lema alikumbusha kuondoka kwa kina Zitto Kabwe na Kitila Mkumbo; kina David Kafulila, kina David Silinde, Dk. Wlborad Slaa na siku za karibuni Mchungaji Peter Msigwa.
Wote hao waliacha maumivu ya aina tofauti ndani ya Chadema, hali ambayo inaonekana kujirudia lakini sasa kwa makundi ya wanachama.
Akizungumza na JAMHURI kuhusu hali ya mambo ndani ya Chadema, Katibu Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Ado Shaibu amesema wao wanamkaribisha mtu yeyote anayetaka kujiunda na chama chao.
“Kuhama chama na kujiunga na chama kingine ni haki ya msingi. Wana haki ya kujiunga na chama chochote wanachoona kinafaa. Kwetu milango iko wazi wakati wowote,” amesema.
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadmu Tanzania (THRDC), Dk. Onesmo Olengurumwa, anasema uamuzi wa wanachama wa Chadema ni sehemu ya demokrasia.
Taarifa zinadai kuwa wimbi lote hilo la wanachama wa Chadema wanaoondoka linatarajiwa kujiunga na Chama cha Ukumbozi wa Umma (CHAUMMA) kinachoongozwa na Hashim Rungwe.
Watanzania wanajiuliza, je, CHAUMMA, baada ya miongo kadhaa ya kuwa chama kisichokuwa na umaarufu mkubwa huku Mzee Rungwe akiwa ndiye pekee anayejulikana nchini, kitaweza kuhimilii misukosuko ya kidemokrasia nchini?
Je, kitafanikiwa vipi kijipanga kitaifa ndaniya muda mfupi kabla ya Uchaguzi Mkuu?