Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Mei 7, mwaka huu, Rais Samia Suluhu ametangaza kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya, kilichotokea asubuhi ya tarehe hiyo katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya moyo.

Akitangaza taarifa hizo, Rais Samia, amesema: “Kwa masikitiko makubwa natangaza kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mzee Msuya kilichotokea leo Mei 7, mwaka huu saa tatu asubuhi katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya moyo. Mzee Msuya ameugua muda mrefu na amekuwa akipatiwa matibabu ndani na nje ya nchi ikiwamo Hospitali ya JKCI, Mzena na kule London, Uingereza.

“Natangaza siku saba za maombolezo ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti kuanzia Mei 7 hadi 13, mwaka huu, taarifa zaidi kuhusu msiba zitaendelea kutolewa na serikali, poleni Watanzania,” anasema.

Baada ya tangazo la kifo hicho, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kimepokea kwa huzuni na masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha mmoja wa waasisi na viongozi waandamizi nchini.

Mei 7, mwaka huu taarifa ya rambirambi ilitolewa na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi.

Anasema Msuya alikuwa miongoni mwa makada na viongozi waliotumikia chama, Taifa letu na nchi yetu, kupitia nafasi alizoaminiwa kwa kuchaguliwa na kuteuliwa, kwa moyo wa dhati, uadilifu wa hali ya juu, na uzalendo usiotetereka.

Pia anasema aliaminiwa kushika dhamana mbalimbali za uongozi katika chama na Serikali, ikiwa ni pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu wa Tanzania na katika nyadhifa hizo, alionyesha uongozi uliotukuka, uliosheheni busara, hekima na kuzingatia maslahi ya wananchi.

“Kwa niaba ya CCM, natoa pole nyingi kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa, marafiki pamoja na Watanzania wote walioguswa na msiba huu mkubwa kwa Taifa letu, kwa namna ya kipekee, tunaungana na Mwenyekiti wa CCM na Rais Samia Suluhu Hassan, katika kipindi hiki cha maombolezo ya siku saba alizotangaza rasmi leo, kwa heshima ya maisha na mchango mkubwa kwa Taifa letu.

“Mzee Msuya ataendelea kukumbukwa kuwa kiongozi aliyeacha alama ya kudumu katika historia ya Tanzania na CCM, Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi, Amina,” anasema.

Kwa upande wake, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Msuya.

Taarifa iliyotolewa Mei 7, mwaka huu na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA, Brenda Rupia, inasema: “Mzee Msuya aliwahi pia kuwa Waziri na Katibu Mkuu katika wizara mbalimbali katika vipindi tofauti vya uongozi wake, CHADEMA tutamkumbuka kwa utumishi wake uliotukuka kwa Taifa letu.

“Tutaendelea kuenzi na kuthamini mchango wake mkubwa katika ujenzi wa Taifa, tutakumbuka pia kauli yake maarufu ndani ya chama chetu aliposema ‘Chadema ni wachambuzi wa mambo’. Kauli iliyobeba heshima na kutambua nafasi ya chama katika mjadala wa kitaifa.”

Kabla mauti hajamfika Mzee Msuya, Mhariri Mwandamizi hapa nchini, Ezekiel Kamwaga, alifanikiwa kufanya naye mahojiano mwaka juzi nyumbani kwake Upanga, Dar es Salaam.

Kupitia mahojiano hayo, Msuya, ametoa siri ya namna ya kudumu madarakani na Watanzania pasipo migogoro; kuwaeleza ukweli.

Katika mazungumzo yake, anasema jambo kubwa alilojifunza kwenye utumishi wake wa umma uliodumu kwa takribani nusu karne, ni kwamba kama watu wakiambiwa ukweli na kuelewa, viongozi hawatakuwa na kitu cha kuhofia.

“Nimejifunza sana kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Mwanzoni mwa miaka ya 1980, tulipitia wakati mgumu sana kiuchumi. Yeye aliita wazee hapa Dar es Salaam na kuwaeleza kwamba hali ni ngumu na tunatakiwa kufunga mikanda.

“Wananchi walimsikia Rais wao akisema hivyo na kwa kweli walimwona naye akiwa amefunga mkanda. Matokeo yake ni kwamba wananchi nao walifunga mikanda kweli kweli na tukapita katika wakati ule mgumu.

“Miaka ya 1980 ilikuwa migumu kwa nchi nyingi za Kiafrika kwa sababu ya masharti yaliyoanza kuwekwa kwetu na vyombo vya fedha vya kimataifa. Wengi wa viongozi katika nchi ambazo raia wake hawakuambiwa nini hasa kinaendelea, waliishia kuondolewa madarakani kwa kuuawa, kupinduliwa au kukimbia. Sisi ukweli wa Baba wa Taifa ulitusaidia,” anasema.

Msuya ni Mtanzania pekee hadi sasa kuwahi kuwa Waziri Mkuu chini ya marais wawili tofauti; Julius Nyerere na Ali Hassan Mwinyi, na katika mazungumzo yake hayo alikiri kwamba nafasi ya Waziri Mkuu na Waziri wa Fedha ni nafasi ngumu kwa mtu yeyote anayekabidhiwa majukumu hayo.

Anasema Tanzania ni nchi kubwa; ikiwa na ukubwa sawa na nchi za Kenya, Uganda na Malawi zikiunganishwa kwa pamoja, na kwamba kazi ya kuwa kiongozi wa mawaziri kwenye kuongoza nchi kubwa namna hiyo na yenye changamoto tofauti si ndogo.

Msuya alikuwa akijibu swali la endapo kuwa kwake Waziri Mkuu – kama ilivyo kwa wanasiasa wengine wote waliowahi kushika wadhifa huo kwenye Serikali ya Tanzania, kilikuwa ni kikwazo kilichosababisha asiweze kuwa Rais wakati alipotaka kuwania nafasi hiyo mwaka 1995.

“Kwanza naamini nafasi ya Urais si nafasi ambayo kila mtu anaweza kuipata. Kuna sababu nyingi zinazosababisha mtu awe au asiwe Rais na si sababu moja tu kwamba labda uliwahi kuwa Waziri Mkuu au Waziri wa Fedha.

“Lakini ni kweli kwamba kama ukiwa Waziri Mkuu na ukatimiza majukumu yako vizuri, uwezekano wa wewe kupishana na mawaziri wenzako au wanasiasa wengine ni mkubwa kuliko ukiwa kwenye majukumu mengine.

“Sasa huwezi kutimiza majukumu uliyopewa na mkubwa wako huku kichwani ukiwaza unataka Urais. Unamwona Rais Samia? Nani alijua kwamba siku moja atakuja kuwa Rais wa Tanzania? Ushauri wangu kwa wanasiasa ni kwamba wao wafanye kazi. Kama Urais utakuja, uje tu,” anasema.

Katika mchakato wa kutafuta mgombea urais ndani ya CCM mwaka 1995, Msuya aliingia katika tatu bora akiwa na Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete – na kumekuwa na maneno ya wachambuzi wengi kwamba ni kura za wafuasi wa Msuya ndizo zilimpa ushindi Mkapa dhidi ya Kikwete wakati huo.

“Mkapa alipigiwa kura na kushinda kwenye mchakato ule kwa sababu waliompigia kura waliona anafaa kupigiwa kura. Hakukuwa na suala la watu wa Msuya kuhamia kwa Mkapa. Hayo ni maneno ya watu tu,” anasema.

Katika mahojiano hayo ya takriban saa nzima, pia alizungumzia suala la utoaji huduma muhimu kama afya na elimu, akisema kimsingi kinachotakiwa kufanywa si kutoa huduma hizo bure bali kuhakikisha kila mtu anachangia kwa kadri ya uwezo wake lakini wale wasio nacho pia wananufaika.

“Unajua kimsingi hakuna kitu kinaitwa elimu bure. Hii ni kwa sababu kuna gharama. Unaingia gharama kujenga majengo, kufundisha na kulipa watumishi, kununua vifaa vya kazi na mambo mengine. Hapo maana yake hakuna bure.

“Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba wenye uwezo wanalipia huduma na wasio na uwezo nao wanapata huduma kama kawaida hata kama hawana uwezo wa kuhudumia. Ndivyo inavyotakiwa kuwa,” anasema.