Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Mwanza

Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limemkamata tena Diana Edward Bundala, maarufu kama Mfalme Zumaridi, kwa tuhuma za kuendesha shughuli za kidini kinyume na sheria, akiwa katika mtaa wa Buguku, kata ya Buhongwa, wilaya ya Nyamagana.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza Mei 15,2025 imeeleza kuwa mtuhumiwa huyo mwenye umri wa miaka 42, amekuwa akitumia makazi yake kama kanisa, ambako amekuwa akihubiri kwa sauti ya juu bila kibali wala usajili, hali ambayo imekuwa ikiwasumbua majirani wa eneo hilo.

Mbali na hilo, Diana anahojiwa pia kuhusiana na video inayoendelea kusambaa kwenye mitandao ya kijamii inayomuonesha akiwa na kundi la watoto wa jinsia zote, huku akidai kuwa yeye ndiye Mungu mwenye uwezo wa kuwatenganisha na kifo. Polisi wamesema uchunguzi bado unaendelea na watashirikiana na taasisi nyingine za serikali ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo nzito.

Hii siyo mara ya kwanza kwa Diana Edward Bundala kutiwa mbaroni mwaka 2021, alikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa kosa la kujitangaza kuwa Mungu na kueneza mafundisho yenye viashiria vya udanganyifu na upotoshaji wa kiimani kwa jamii.

Pia, alihusishwa na kuwahadaa waumini wake kwa kuwataka watoe mali zao kwa imani kuwa watapokea miujiza. Katika kesi hiyo ya awali, alifikishwa mahakamani jijini Mwanza lakini aliachiwa kwa dhamana huku akitakiwa kutojihusisha tena na shughuli hizo hadi kesi itakaposikilizwa na kuamuliwa.

Jeshi la Polisi limewataka wananchi wenye taarifa zozote zitakazosaidia uchunguzi kufika mbele ya vyombo vya dola. Polisi wametoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano huku wakiahidi kuchukua hatua kali za kisheria pindi uchunguzi utakapokamilika.