Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla, ametoa kauli yenye msisimko kuhusu kile anachokiita “kutimia kwa utabiri wa Tundu Lissu”, Mwenyekiti wa CHADEMA, kuhusu hali ya chama chake.
Akizungumza katika mkutano huko Kilosa, Makalla alielezea furaha yake kwa kile alichokiita kuanguka kwa CHADEMA kutokana na hamahama ya viongozi waandamizi wa chama hicho, hususan wale wanaohusishwa na kundi la G55. Alidai kuwa hali hiyo ni matokeo ya matamshi ya Lissu na Makamu wake, John Heche, ambao waliwahi kusema kuwa “watakinukisha”.
“Walisema tutakinukisha, na ni kweli wamekinukisha CHADEMA. Hongera sana Lissu na Heche, kauli yao inafanya kazi vizuri – chama kinasambaratika,” alisema Makalla kwa msisitizo.
Makalla aliongeza kuwa hali ya sasa ya CHADEMA imesababisha kudhoofika kwa chama hicho kiasi cha kushindwa kushiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba. Alidai kuwa chama hicho kimepoteza mwelekeo na uwezo wa kushindana kisiasa kwa sasa.
“CHAMA kimesambaratika, viongozi wanahama kila kukicha. Hakina tena nguvu ya kushiriki uchaguzi.”
Hata hivyo, ni vyema kukumbuka kuwa mvutano ndani ya CHADEMA uliibuka baada ya chama hicho kutangaza kutoshiriki uchaguzi mkuu na pia kususia kusaini maadili ya uchaguzi. Viongozi waliotangaza kujiondoa wamedai kuwa uamuzi huo wa chama umewanyima fursa ya kushiriki mchakato wa kidemokrasia.
Katika hali inayoashiria mgawanyiko wa ndani, baadhi ya wanachama na viongozi wa kundi la G55 walilalamikia maamuzi ya chama na kutangaza kujiondoa, wakitaja sababu mbalimbali ikiwemo kunyimwa nafasi za kugombea.
Taarifa hii inaonyesha taswira ya mabadiliko ya kisiasa ndani ya CHADEMA, huku CCM ikitumia fursa hiyo kuonesha ukomavu wa kisiasa na kuzidi kujiimarisha kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
