▪️Nishati ya umeme wa jua kupunguza gharama za uzalishaji kwa asilimia 65 migodini

▪️Aelekeza kufanyika mradi wa majaribio kwa wachimbaji wadogo

▪️Aipongeza Kampuni ya Madini Taur kwa matumizi ya Nishati safi na kupanua shughuli za mgodi

Igunga,Tabora

Imeelezwa kuwa mradi unaotumia teknojia ya kisasa ya uzalishaji umeme wa jua ni mkombozi kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini kwa kupunguza gharama za uzalishaji kwa zaidi ya asilimia 65.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde leo Mei 18, 2025 wakati akizindua mradi wa uzalishaji umeme wa jua uliopo katika kijiiji cha Nanga Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora ambao umesimikwa na Kampuni ya Uchimbaji madini ya Taur Tanzania.

Amesema kuwa, mradi wa uzalishaji umeme wa jua unaunga mkono juhudi za Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan za kuhamasisha matumizi ya Nishati safi na kupambana na uchafuzi wa mazingira nchi kwa kupunguza matumizi yanayosababisha hewa ya ukaa.

Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde amesema teknojia hiyo ya uzalishaji umeme wa jua itapelekwa katika maeneo mengine ya uchimbaji kwa lengo la kuwasaidia wachimbaji wadogo katika maeneo yao ili wachimbe kwa tija na kuchochea uchumi wa Taifa pamoja na kulinda mazingira.

Aidha, Mavunde amesema Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amefanya makubwa katika kuiendeleza Sekta ya Madini ambapo mpaka sasa sekta imeweza kuchangia katika pato la Taifa kwa asilimia 10.1 mwaka 2024 ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya lengo la mwaka 2025 kama ilivyoelekezwa na Ilani ya Uchaguzi na Mpango wa Maendeleo wa miaka 5.

Pamoja na mambo mengine, Waziri Mavunde amesema, katika mikoa ya Dodoma, Singida na Tabora kuna miradi mikubwa ya Utafiti inaendelea katika maeneo hayo ambapo kuna uwezekano mkubwa wa kuanzishwa kwa mgodi mkubwa utakaopelekea kubadilisha maisha na uchumi wa watu katika maeneo hayo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Igunga Sauda Mtondoo amesema uwepo wa Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Taur Tanzania Limited wilayani Igunga umeleta maendeleo makubwa katika kijiiji cha Nanga na Wilaya ya Igunga kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kuleta ajira na kukuza uchumi kwa jamii inayozunguka Mgodi.

Mtondoo amesema Mwaka 2023/24 Wilaya ya Igunga ilizalisha zaidi ya Kilo 400 za dhahabu na kuanzia June 2025 mpaka May Mwaka 2025 Igunga imeshazalisha zaidi kilo 300 za dhahabu, ambapo pia, ametumia fursa hiyo kumuomba Waziri Mavunde kupatiwa Soko la Madini wilayani Igunga.

Naye, Meneja Mkuu wa Kampuni ya Taur Tanzania Limited Martin George amesema Kampuni hiyo imeanza shughuli za kuchenjua Madini Mwaka 2010 kwa kutumia Nishati ya mafuta (jenereta) na baadae umeme wa tanesco hivyo amesema teknojia ya uzalishaji umeme kwa kutumia jua umesaidia kupunguza gharama za uzalishaji kwa kiwango kikubwa.