Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema Serikali inatekeleza Mradi wa kuimarisha uwezo wa jamii za pwani kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Tabianchi katika visiwa vya Unguja na Pemba wenye thamani ya Dola za Marekani milioni moja (shilingi bilioni 2.7).

Amesema mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Mamlaka ya Usimamizi wa Mzingira Zanzibar (ZEMA).

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akijibu maswali wakati wa Kikao cha 28 cha Mkutano 19 wa Bunge jijini Dodoma leo tarehe 20 Mei, 2025.

Mhe. Khamis ametoa kauli hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Donge Mhe. Mohammed Jumah Soud aliyeuliza kwanini NEMC haianzishi utaratibu wa kuishirikisha ZEMA ili kuongeza ufanisi wa uibuaji na usimamizi wa miradi ya mazingira Zanzibar.

Akiendelea kujibu swali hilo, Naibu Waziri Khamis alisema ili kuongeza ufanisi katika uhifadhi na usimamizi wa mazingira katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumekuwa na utaratibu wa ushirikiano kati ya NEMC na ZEMA katika uibuaji na usimamizi wa miradi ya mazingira.

Alisema miradi miwili inayoandaliwa kwa ushirikiano wa taasisi hizo mbili ni Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi katika maeneo yenye upungufu wa maji baridi.

Mhe. Khamis alifafanua kuwa mradi huo upo katika hatua za kupata kibali cha fedha kutoka Mfuko wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (AF) na unatarajiwa kutekelezwa Unguja na Pemba kwa thamani ya Dola za Marekani milioni 3.5 (shilingi bilioni 9.5).

Halikdhalika, alibainisha kuwa Mradi wa Kuimarisha Miundombinu katika Ukanda wa Pwani ili Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi upo katika hatua za kupitishwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) na uunatarajiwa kutekelezwa Tanzania Bara na Zanzibar.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Khamis alisema kupitia bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais ya mwaka 2025/26 Serikali inatarajia kutatua changamoto ya maji ya bahari kuingia kwenye makazi ya wananchi.

Alisema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Nungwi Mhe. Simai Hassan Sadiki aliyeyaka kufahamu lini NEMC na ZEMA zitakuwa na ushirikiano ili kuondosha maji ya bahari yanayoathiri maeneo ya pwani yakiwemi Zanzibar.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akiteta jambo na Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi wakati wa Kikao cha 28 cha Mkutano 19 wa Bunge jijini Dodoma leo tarehe 20 Mei, 2025.