Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi, ameshuhudia utiaji saini wa mkataba wa mkopo wa Shilingi Bilioni 240 kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Benki ya CRDB kwa ajili ya ujenzi wa skuli 23 za kisasa za ghorofa hapa nchini.
Hafla hiyo imefanyika Ikulu ambapo Benki ya CRDB imewakilishwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Abdulmajid Nsekela na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi – Afisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dk Juma Malik Akil.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Dk Mwinyi amesema mkataba huo ni hatua kubwa kwa Zanzibar ambayo kwa mara ya kwanza imefanikiwa kupata mkopo mkubwa kutoka nje ya nchi bila ya kuwa na dhamana ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuwezeshwa na benki za ndani ya nchi tangu Mapinduzi ya mwaka 1964.
Dk Mwinyi ameeleza kuwa mkopo huo wa Euro milioni 79 (sawa na Shilingi Bilioni 240) utatumika kujenga skuli za kisasa za ghorofa 23 katika maeneo yenye uhitaji mkubwa wa skuli Unguja na Pemba.
Aidha, amebainisha kuwa mkopo huo umewezeshwa kupitia ushirikiano wa Benki ya CRDB na Benki ya Udachi (Deutsche Bank), kwa dhamana ya Bima ya CESCE kutoka Uhispania. Fedha hizo zitatumika pia kununua vifaa vya kisasa vya Maabara, Maktaba, Kompyuta, na Samani.
Amesema kwa muda mrefu, Serikali ilikuwa na njia mbili pekee za kupata mikopo kwa kupitia dhamana ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au kutegemea bajeti za ndani ambazo zote zilichukua muda mrefu na kuchelewesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Kupitia mpango huo mpya, Dk Mwinyi amesema Zanzibar sasa inaweza kutekeleza miradi mingi ya kimkakati kwa haraka ndani ya kipindi cha miaka mitano ijayo.
Akitaja baadhi ya miradi ya kimkakati itakayotekelezwa ndani ya miaka mitano ijayo, Mwinyi amesema itajumuisha ujenzi wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani, Uwanja wa Ndege wa Pemba, barabara za Chake Chake–Mkoani, Kisauni–Fumba, Uwanja wa Soka wa kisasa wa michuano ya AFCON 2027, Uwanja wa Ndege wa Pemba na Hospitali za Mikoa.

