Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salam
Mwezi huu Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imezindua rasmi Sera Mpya ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2024. Kwa mtu anayechukulia diplomasia kama kazi ya mabalozi tu, anaweza asione uzito wa jambo hili. Lakini kwa anayefuatilia mwelekeo wa taifa letu katika ulimwengu unaobadilika kwa kasi, hili ni tukio la kihistoria na la kujivunia.
Tofauti na sera ya mwaka 2001 iliyozingatia zaidi masuala ya diplomasia ya uchumi kwa nchi, sera mpya imebeba msukumo wa diplomasia inayogusa maisha ya watu. Pamoja na kuweka msingi wa kuchochea biashara, uwekezaji, utalii, na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kutangaza fursa za Tanzania, sera hii imewakumbuka ndugu zetu wa diaspora, bila kusahau Watanzania waliokuwa wanaota kwenda nje ya nchi na kufanya huko kwa miaka mingi iliyopita.
Sitanii, kwa mara ya kwanza sera hii inaweka mbele diplomasia ya matokeo. Inatambua kuwa ubalozi ni kichocheo cha maendeleo ya ndani. Haifai tu kuwa na balozi nje ya nchi, bali balozi huyo sasa atapimwa kwa uwezo wake wa kufungua masoko, kuvutia wawekezaji, kutafutia Watanzania fursa za kufanya kazi nje ya nchi, kukusanya watu wenye vinasaba na Tanzania kurejea na kuwekeza nchini, huku ikitangaza bidhaa za Tanzania kimataifa.

Sera hii inalenga kuwapa hadi maalum Watanzania wanaoishi nje ya nchi. Kwa uzinduzi wa sera hii, Watanzania hawa sasa wataweza kutoka na kuingia nchini bila visa, wakati Sheria ya Ardhi na Sheria ya Uhamiaji zitabadilishwa. Diaspora wataruhusiwa kumiliki ardhi ambayo ni nguzo ya msigi katika uwekezaji kwa sehemu yoyote duniani.
Nimepata fursa ya kutembelea nchi mbalimbali, wenzetu hawa wanaoishi nje ya nchi, si kwamba wanapapenda. Kiuhalisia ukiwasikiliza na ukizungumza nao, mapenzi yao makubwa yapo hapa Tanzania. Mimi nimepata fursa ya kusoma Uingereza na namshukuru Mungu nimetembelea mabara yote ya dunia hii kwa maana ya Asia, Ulaya, Amerika ya Kusini, Amerika ya Kaskazini na nchi nyingi za Afrika.
Sitanii, ninayoandika haya nimeyaishi. Nchi za ughaibuni zina utamaduni tofauti mno na wa kwetu Tanzania. Ndugu zangu, mimi nasikiliza siasa zetu hapa nyumbani. Anasimama mtu anasema hakuna maendeleo. Nafahamu wanaofanya siasa wanajua kuwa hili watu wanapenda kulisikia na linawasaidia kupata kura zinazowaletea kula.
Tukienda kwa majirani zetu hapa Afrika Kusini, jamii inatumia bucket system (mtondoo) kuhifadhi haja kubwa ndani ya nyumba zao na halmashauri ya Jiji au Mji inapita kila Jumamoshi kutapisha ndoo na kwenda kumwaga uchafu. Hawajui kuchimba choo maana yake ni nini. Sisi Tanzania tumeivuka kitambo hatua hii. Hakuna mtu anayelala na mtondoo ndani mwake. Hata watani zangu, angalau wanakwenda vichakani!!!
Huko nje kuna utengano mkubwa wa kijamii (social isolation). Ukienda nchi za Ulaya au Amerika mnatambuliwa kwa rangi zenu na haki zinapatikana kwa mkondo huo huo kimyakimya. Utaambiwa huyu ni Mmarekani Mweusi, huyu ni Mwarabu, huyu ni Mzungu Mweupe, huyu ni Mhindi… sisi hapa tumevuka kitambo.

Hata kazi wanazofanya ni hizo hizo. Weusi (Africans) kazi zao nyingi ni kuburudisha Wazungu. Utawakuta kwenye michezo kama ya basketball, baseball, kurusha mikuki, viwandani kwenye kazi za mitulinga… Ndugu zetu hawa wanaoishi Ulaya, Asia na Amerika waulize kama kuna meneja wa benki, mkurugenzi wa kampuni ya data, mmiliki wa hoteli ya nyota tano, mkuu wa idara hospitalini… taja kada zote.
Sitanii, wakati nasoma shahada ya uzamili Uingereza, kuna Watanzania wenzangu, Waghana na Wanaigeria, niliwambia turejee nyumbani, wakaniambia waache kazi rahisi za kufunga makasha ya vyakula, perfume, ulinzi na nyingine zinazolipa kwa pauni (pound) warejee Tanzania na nchi zao nyingine kutafuta kazi wasiyokuwa na uhakika nayo? Waliniambia wataanza kidogo kidogo wakiishazoea Uingereza watakuwa mameneja. Leo ni karibu miaka 20 tangu tumemaliza masomo, sijasikia aliyepanda hata kuwa Afisa Mwandamizi.
Sana sana wakirejea hapa Tanzania, wakija kunitembelea nyumbani, ukiwakaribisha kwako wanakiri kuwa Ulaya wamepoteza muda. Nawauliza kama waliishajenga, wananiambia bado wanaishi kwenye studio (Ulaya – chumba ndo sebule, ndo chumbani pa kulala). Hata hivyo, hakuna ubishi kuwa kwa kuosha wazee, kulinda na kufanya kazi viwandani wanapata fedha ndefu, ila uko wapi utu wao na matumizi ya elimu yao? Hawa sasa wanapatiwa haki ya kurejea, wawekeze nyumbani Tanzania. Wafanye kazi kama watumwa ughaibuni, hapa nyumbani Tanzania waishi kama wafalme.
Sitanii, faida nyingine ya sera hii mpya ni kuweka mkazo kwenye kukuza Kiswahili. Inakwenda kubidhaisha Kiswahili kiwe lugha ya dunia. Mkazo unaowekwa katika Kiswahili unadhihirisha kuwa Tanzania sasa inakwenda kuwa kiongozi wa kweli katika Kiswahili, kwani sera yetu inakitambua Kiswahili kama bidhaa ya kuuzwa kimataifa sasa. Hii ni fursa pia ya kuajiri watu wetu kwenda kufundisha Kiswahili.
Nilikuwa pale Zimbabwe hivi karibuni, nikaona Kiswahili kinachofundishwa na watu wanakipenda. Wanataka kufahamu jinsi ya kujitambulisha. Mtu ajue kusema mimi ni Mzimbabwe au Mtanzania. Jina langu ni Balile. Natokea Bukoba, ila naishi Dar es Salaam. Kila siku naamka saa 11 alfajiri, napiga mswaki, nafanya mazoezi, baada ya hapo nakunywa chai na kwenda kazini… wao hawadai kufahamu Kiima, Kiarifu, Kishazi au Shamilisho. Wanataka kufahamu lugha ya kuzunguza na wanafurahi sana wakiweza kutamka maneno ya Kiswahili. Hii Watanzania wengi wanaweza kuifundisha sehemu mbalimbali duniani. Ni fursa ya ajira.

Sera hii mpya pamoja na mambo mengine, inajikita katika kukuza uchumi wa buluu. Uchumi wa buluu si kwenye bahari pekee, hata kwenye maziwa na mito mikubwa tunakwenda kupata wawekezaji kupitia sera hii. Kwa hakika, hii nayo inakwenda kuongeza ajira. Si kwamba sera hii imehama kabisa katika yale majukumu ya kimataifa ya ulinzi na usalama, ujirani mwema, kusaidia wahitaji na mengine, ila sera hii inakuwa dira kwa Mtanzania wa kawaida kuanzia diaspora hadi Mtanzania aliyepo hapa nchini.
Sitanii, sera pia imeweka bayana umuhimu wa ushirikiano wa kikanda na kimataifa unaolenga maslahi ya taifa. Hili lina maana kwamba Tanzania itajenga mahusiano ya kimkakati, si kwa misingi ya urafiki wa kihistoria tu, bali kwa kuzingatia faida zinazotokana na ushirikiano huo kwa wananchi wake.
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, katika hili imewatendea haki Watanzania. Diplomasia sasa si anasa tena, ni nyenzo ya maendeleo. Tuna kila sababu ya kuipongeza serikali kwa kuja na dira hii mpya, na ni wajibu wetu sisi wananchi – hususan sekta binafsi – kuielewa na kuichangamkia kwa vitendo.
Sitanii, Tanzania haiwezi kujitenga na dunia. Dunia nayo haiwezi kuijua Tanzania kama hatujitangazi. Sera hii mpya ni daraja kati ya tunakotoka na tunakotaka kufika. Huu si wakati wa kukaa kimya. Ni wakati wa kuungana kuipeleka Tanzania mbele kupitia sera hii mpya na kushuhudia matokeo makubwa kwa Watanzania. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404827