*Majengo ya mamilioni yatelekezwa, yageuka magofu

*Askari Uhifadhi walala vichakani mithili ya digidigi

*Ukata wasababisha ujangili kuibuka upya Pololeti, Serengeti

*Nyamapori zauzwa nje nje migahawani Loliondo

Na Mwandihi Wetu, JamhuriMedia, Loliondo

Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) ambayo imepewa usimamizi wa Pori la Akiba la Pololeti mkoani Arusha, imelemewa na jukumu hilo.

Kutokana na hali hiyo, NCAA imeshindwa kukamilisha majengo ya makazi na ofisi ambayo ujenzi wake ulianza baada ya mwekezaji kutoa msaada wa mamilioni ya fedha kwa kazi hiyo.

JAMHURI limefika eneo hilo na kushuhudia majengo yaliyojengwa kwa mawe yakiwa yametelekezwa na kuwa magofu.

Askari wachache wa Jeshi la Uhifadhi waliopo eneo hilo, wanalazimika kulala kwenye magofu hayo kwa kuunga vipande vya maturubai na mabati.

Wanaishi katika mazingira magumu mno kwenye eneo la Meremi Iloingok lililoko kilometa chache kutoka mpaka wa Tanzania na Kenya.

Msemaji wa NCAA, Hamis Dambaya, ameliambia JAMHURI kuwa suala hilo la magofu, uongozi wa Mamlaka unalijua, na hatua za kukamilisha ujenzi zitaanza karibuni.

Mazingira wanamoishi askari hao yanatajwa kuwa miongoni mwa sababu za kuwapo taarifa zisizotiliwa shaka kwamba yanachangia, ama wao kusukumwa na hali hiyo na hivyo kushiriki vishawishi vya kukiuka maadili, au kuwafanya washindwe kutekeleza wajibu wao na hivyo kutoa mwanya kwa majangili kufanya uhalifu kwa kuua wanyamapori katika Pori la Akiba Pololeti.

Tayari kumeripotiwa kuwapo ujangili katika eneo karibu lote la magharibi mwa Pololeti na Mashariki mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Kama ilivyo Pololeti kunakosimamiwa sasa na NCAA, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti nako kunaripotiwa kuwapo matukio ya ujangili kutokana na askari kutolipwa posho kunakosababishwa na ukata unalolikumba Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).

Inaelezwa kuwa askari wa TANAPA, tofauti na zamani ambako walilipwa stahili zao ikiwa pamoja na motisha kwa kukamata majangili na mitego, kwa sasa malipo yao yamekuwa shida, na vivutio kama motisha vimeondolewa.

“Unaweza kuona kuwa TANAPA wana hali ngumu, huku NCAA hawatoshi, lakini nao wana hali ngumu. Hapa ndipo kwenye mwanya wa ujangili na uingizaji mifugo hifadhini. Wakubwa wanajifanya hawajui, lakini nikuhakikishie kuwa hizi hifadhi zinamalizwa na ujangili,” kimesema chanzo chetu.

Katika Pololeti, hali hiyo imesababishwa na kufutwa kwa kikosi cha doria kilichokuwa kikigharimiwa na mwekezaji, kampuni ya Ortello Business Corporation (OBC). Kikosi hicho ambacho kilishirikiana na askari wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) na vikosi vingine, kilifutwa kwa kuwa NCAA hawana utaratibu huo.

Hadi kinafutwa, OBC walikuwa wakitumia Sh milioni 54 kila mwezi kugharimia magari manane ya doria na askari 48. OBC wanasema wako tayari kuendelea kushiriki doria kwa kutoa wafanyakazi, magari na vitendea kazi vinavyohitajika ili pamoja na mamlaka za serikali waweze kulinda rasilimali zilizopo.

“Sisi tuko tayari kabisa. Tuliondoa kikosi kwa sababu tuliambiwa kuwa kazi ya doria ni ya NCAA, lakini sasa hali inaonekana ni mbaya. Tutambuliwe kuwa sisi ndiyo wawekezaji kwenye hiki kitalu. Tupewe ushirikiano na stahiki za kisheria bila kuwekewa watu wengine, jambo ambalo linakinzana waziwazi na sheria,” wamesema OBC.

Kukosekana kwa kikosi kumetoa mwanya wa ujangili kushamiri hasa katika maeneo ya Leng’usa, Mlima Kuka (mpakani mwa Tanzania na Kenya), na eneo la Malambo. Hapo Malambo nyama nyingi huandaliwa na kusafirishwa kwenda kuuzwa eneo la Shombole nchini Kenya.

Si hivyo tu, bali nyamapori sasa inauzwa nje nje katika maeneo ya Wasso na Loliondo kwa kuwa upatikanaji wake umerahisishwa na kuachwa kwa eneo la kilometa za mraba 2,500 bila uangalizi rasmi wa mamlaka za kisheria kama ilivyokuwa awali wakati kukiwa na Pori Tengefu la Loliondo chini ya TAWA.

“Hapa nyama ya porini siyo shida, tena hawa wakubwa wenyewe ndiyo wakati mwingine wanasambaza, ninakuhakikishia hakuna mkubwa hapa Loliondo ambaye hali nyama ya pori, hao ndiyo wanaoongoza,” kimesema chanzo chetu.

Uwepo wa nyamapori migahawani na kwa wananchi kunathibitisha kuwa inapatikana kwa njia haramu kwani eneo hilo halina uwindaji wa wenyeji wa kisheria kama yalivyo maeneo mengine nchini.

Swali linaloulizwa ni kwamba, kwa nini wanaohusika na hujuma hizi hawakamatwi licha ya kuwapo maofisa wanyamapori Loliondo? “Maofisa wanyamapori hapa ni wa kabila la jamii hii hii, hawa wanajuana. Hawawezi kuwakamata ndugu zao, ni kama polisi apelekwe kijijini kwao – unadhani atamkamata ndugu yake?

“Mara zote tumeshauri mabwana nyama wa hapa waletwe watu ambao si wazawa wa huku, hao watafanya kazi bila woga, lakini hawa hawawezi kuwakamata ndugu zao. Isitoshe wamekaa muda mrefu sana hapa tangu mimi nikiwa mwanafunzi wa sekondari,” amesema mtoa taarifa wetu.

Hivi karibuni watu kadhaa wamekamatwa eneo la Malambo wakiwa wameua twiga. Twiga ni mnyama asiyewindwa kisheria kutokana na kutambuliwa na kuenziwa kama alama ya taifa la Tanzania. Maeneo yote haya yako ndani ya Pori la Akiba la Pololeti yanayopakana na Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Maeneo yote hayo yameenea mitego ya waya inayowekwa na majangili. Wiki iliyopita askari wachache wa doria walichoma kambi ya majangili iliyo mpakani mwa Pololeti na Serengeti.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa kukosekana kwa ushirikiano kati ya NCAA na OBC kumesababisha barabara nyingi zikose matengenezo hivyo kufanya kazi ya doria iwe ngumu na kutofikika maeneo mengi.

Licha ya kuwapo kampuni nyingine mbili za uwekezaji -kinyume cha sheria- ndani ya Pori la Akiba Pololeti, kampuni hizo hazijishughulishi na, ama utengenezaji miundombinu ya barabara, na au doria dhidi ya ujangili na majangili.

Kampuni hizo zinaendelea kutumia eneo la Pori la Akiba ambalo kisheria amekabidhiwa mwekezaji OBC na ndiye anayelipa ada, kodi na tozo mbalimbali kwa mujibu wa sheria.

Kampuni hizo zinaingiza watalii wake ndani ya Pololeti na katika maeneo jirani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti ilhali kukiwa hakuna lango mahsusi la kukusanya maduhuli kama ilivyo kwa NCAA, Hifadhi ya Taifa Serengeti, na maeneo mengine nchini.

Zipo taarifa za uhakika kuwa baadhi ya watalii kutoka Kenya wamekuwa wakiingizwa, hasa nyakati za usiku na wanaowawezesha kufanya hivyo ni baadhi ya watumishi wa NCAA ambao majina yao tunayahifadhi kwa sasa kwa kuwa JAMHURI halijazungumza nao.

Pia waangalizi hao wa NCAA licha ya kutambua kuwa Sheria ya Uhifadhi Na. 5 ya mwaka 2009 na Kanuni zake zinazuia shughuli za kibinadamu ndani ya Mapori Tengefu, hali imekuwa sivyo kwa Pori la Akiba la Pololeti.

Kampuni ya AndBeyond ambayo uwekezaji na uhalali wake vinahojiwa kwa misingi ya kisheria kwenye pori hilo, imeachwa iendelee na kilimo cha mbogamboga ndani ya Pori la Akiba.

Hadi wiki moja iliyopita, kilimo hicho kilikuwa kinaendelea, lakini baada ya JAMHURI kuwahoji viongozi wa NCAA na Wizara ya Maliasili na Utalii, mazao hayo yameng’olewa.

Msemaji wa NCAA, Dambaya amesema: “Hili la bustani sina taarifa nalo, naomba uniachie nilifuatilie.”

NCAA pia imeingia kwenye mgogoro na Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro baada ya kushindwa kuwalipa gawio la kisheria la asilimia 25 ya mapato yanayotokana na uwekezaji Pololeti.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Marekani Bayo, anasema ni miaka minne sasa NCAA imegoma kuwalipa gawio, ilhali kila mwaka Mamlaka hiyo inapokea zaidi Sh bilioni 1 kutoka OBC.

“Uhusiano kati ya wasimamizi wa pori na sisi si mzuri. Awali pori likiwa chini ya TAWA tulikuwa tunapokea asilimia 25, lakini tangu NCAA wamepewa huu ni mwaka wa nne hatupewi chochote.

“Kwa maoni ya Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro na Kamati ya Fedha, tunapendekeza bora hili pori linarudi katika usimamizi wa TAWA kwa sababu NCAA hawatupi chochote.

“Sisi tunatamani sana tuwe na uhusiano unaoleta manufaa kwa msimamizi wa pori na wananchi wa Ngorongoro kwa sababu pori lipo Ngorongoro, na wananchi wanastahili kunufaika nalo. Kwa ufupi niseme Mamlaka hawana uhusiano mzuri na Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro,” anasema Bayo.

Mmoja wa viongozi wa NCAA ameliambia JAMHURI: “Si kwamba hatutaki kuwalipa, bali kikwazo kipo Hazina. Fedha zote zinaenda Hazina, na sisi tunalazimika kupokea fedha ili tuendeshe mambo, sasa kama wao hawarudishi, sisi tufanyeje?”

Ameulizwa kwa nini wanapoomba fedha za matumizi wasitumie nafasi hiyo kuomba ile asilimia 25 ya Halmashauri, akajibu: “Nadhani hilo linafanyiwa kazi, waambie wasubiri.”

Urasimu/mgongano

Kisheria mapori, yakiwamo ya akiba yanatakiwa yawe chini ya usimamizi wa TAWA. Hata hivyo, kinyume cha sheria hiyo, NCAA imepewa jukumu hilo kwa kile ambacho aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Angela Kairuki, aliliambia JAMHURI kuwa ulikuwa uamuzi wa Baraza la Mawaziri.

Uamuzi huo unatajwa kuleta changamoto nyingi katika uhifadhi wa eneo hilo muhimu.

Kuna hoja nzito kwamba NCAA haina utaalamu wa kutosha kusimamia pori kama Pololeti. Hii ni kutokana na ukweli kwamba jukumu lao la msingi limejikita zaidi katika kusimamia maeneo ya uhifadhi mseto na utalii, badala ya kusimamia mapori ya akiba.

Kwa upande mwingine, TAWA imebobea katika kusimamia mapori ya akiba, ikiwa na rasilimali watu na vifaa maalumu vya kukabiliana na changamoto za uhifadhi katika maeneo hayo.

Kwa upande wa vitendea kazi, NCAA inakabiliwa na upungufu wa magari ya doria, hali ambayo kwa kiasi kikubwa uimeathiri wezo wa kudhibiti ujangili ambao sasa umeshamiri katika eneo la Pololeti.

Urasimu katika utaratibu wa kutoa vibali

Hali imekuwa mbaya kutokana na urasimu uliopo katika utoaji vibali kwa mwekezaji. Mfumo wa sasa unamlazimisha mwekezaji kuomba vibali kupitia NCAA, kisha NCAA nayo kupeleka maombi hayo kwa TAWA ili kupata idhini, na hatimaye TAWA kutoa majibu kupitia NCAA.

OBC wanasema utaratibu huu wa kurudisha maombi na majibu unachukua muda mrefu na unakatisha tamaa mwekezaji; jambo ambalo linapunguza motisha ya kushiriki katika uhifadhi na uwekezaji katika pori hilo.

Ujangili na utalii wa kinyemela

Moja ya athari kubwa ya ukosefu wa usimamizi bora ni kushamiri kwa ujangili katika eneo la Pololeti. Ujangili umekuwa tatizo sugu, huku ikiripotiwa kuwa baadhi ya watumishi wa NCAA wanahusishwa na vitendo hivyo.

Majangili wanajihusisha na uwindaji haramu wa wanyama na kuuza nyama pori katika migahawa mbalimbali ya Loliondo na maeneo mengine ya jirani.

Mbali na ujangili, kuna pia utalii wa kinyemela unaofanywa na watalii kutoka Kenya ambao huingizwa mchana na usiku katika eneo la Pololeti.

Utalii huu wa kiholela unafanyika kwa kukwepa ada na tozo mbalimbali za utalii ambazo zingepaswa kulipwa NCAA na serikali kuu.

Pori la Akiba la Pololeti limekuwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa doria za mara kwa mara. Askari wa uhifadhi licha ya kuwa ni wachache, wanakosa vifaa vya msingi na sehemu bora za kuishi. Kwa sasa, askari wengi wanaishi katika mahema, hali inayowafanya kukosa motisha na ufanisi katika kazi zao. Eneo ambalo linapaswa kuwa kambi ya askari limeachwa na kuwa magofu, hali ambayo inazidi kudhoofisha juhudi za uhifadhi; ilhali wakubwa wao wakiishi katika nyumba nzuri na magari Loliondo.

Ukosefu wa doria umechangia ongezeko la ujangili na shughuli nyingine haramu zinazotishia uhai wa wanyamapori. Kwa kuwa eneo hilo halina ulinzi wa kutosha, ni rahisi kwa majangili na wahalifu wengine kuingia na kutoka bila kugunduliwa. Hali hii inatishia uendelevu wa uhifadhi wa wanyamapori na ulinzi wa maliasili katika eneo hilo.

Mapendekezo ya wadau

Kurejesha Usimamizi kwa TAWA: inapendekezwa kuwa ili kuboresha usimamizi wa Pori la Akiba la Pololeti, ni vyema kuzingatia sheria ya uhifadhi inayotaka mapori tengefu na mapori ya akiba kuwa chini ya TAWA.

Wanasema kurudisha usimamizi kwa TAWA kutaleta utaalamu na kuimarisha juhudi za uhifadhi, kwani TAWA ina utaalamu wa kusimamia mapori hayo; lakini pia Halmashauri italipwa gawio la asilimia 25 ambalo ni takwa la kisheria.

Kudhibiti ujangili na utalii wa kinyemela: Serikali inashauriwa kuanzisha operesheni za mara kwa mara za kudhibiti ujangili na kusimamia kwa karibu mpaka ili kuzuia utalii wa kinyemela.

Kuboresha makazi na motisha kwa askari wa uhifadhi: Kuwekezwa katika ujenzi wa kambi za kisasa kwa askari wa uhifadhi ni hatua muhimu. Hii itasaidia kuwapa askari mazingira bora ya kuishi na kuongeza motisha ya kufanya kazi kwa ufanisi katika kulinda wanyamapori na maliasili za Pololeti.

“Uamuzi wa kuipa NCAA jukumu la kusimamia Pori la Akiba la Pololeti ni kinyume cha sheria za uhifadhi, na umesababisha changamoto nyingi katika utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi. Ukosefu wa utaalamu, vitendea kazi, na urasimu katika utoaji wa vibali vimepunguza ufanisi wa usimamizi wa pori hili, huku ujangili na utalii wa kinyemela vikiongezeka.

“Ni muhimu kuchukua hatua za haraka na madhubuti kurekebisha changamoto hizi ili kulinda maliasili na kuhakikisha uendelevu wa uhifadhi katika eneo la Pololeti,” amesema mmoja wa waliowahi kuwa Wakurugenzi wa Idara ya Wanyamapori.