Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia l, Dodoma

Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), imetangaza kuongezeka kwa bajeti ya mikopo kwa vyuo vya elimu ya juu kutoka Shilingi bilioni 570 hadi bilioni 787 katika kipindi cha miaka minne, hatua iliyowezesha ongezeko la wanufaika kwa asilimia 39.6.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, ameeleza hayo leo Mei 27,2025 Jijini Dodoma wakati akieleza maganikio ya Wizara hiyo na kueleza kuwa hatua hiyo ni mafanikio makubwa katika sekta ya elimu .

Prof. Mkenda amesema mafanikio hayo yanatokana na dhamira ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuwekeza katika maendeleo ya rasilimali watu kupitia elimu bora na teknolojia ya kisasa na kwamba mwelekeo huo umekuwa msingi wa maboresho makubwa yanayoendelea katika sera, mitaala na mifumo ya elimu nchini.

Katika kulinda ubora wa elimu sambamba na upanuzi wa fursa, Waziri amesema serikali imepitisha toleo jipya la Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, ambalo linapanua elimu ya lazima hadi miaka 10.

Amesema Mitaala kuanzia elimu ya awali hadi vyuo vya ualimu imeboreshwa ili kutoa maarifa, stadi na ujuzi unaozingatia biashara, historia ya taifa, lugha, pamoja na vipaji na vipawa vya wanafunzi.

“Mageuzi haya ya kimkakati yamekwenda sambamba na mapitio ya Sheria ya Elimu Sura ya 353 na uanzishaji wa mifumo ya kisasa ya kidigitali,aidha mfumo wa kitaifa wa takwimu za elimu (ESMIS) pamoja na mfumo wa tathmini ya ujifunzaji kwa njia ya kidigitali umeanzishwa ili kuongeza ufanisi na uwazi katika upangaji wa sera na utekelezaji wake, “amesema

Kwa upande wa elimu ya juu, kupitia Mradi wa Higher Education for Economic Transformation (HEET), Prof. Mkenda amefafanua kuwa Serikali imeanzisha kampasi 16 mpya, ikiwemo visiwani Zanzibar, na kuongeza idadi ya wahadhiri wanaopata mafunzo ya juu.

Amesema Serikali pia imeanzisha mikopo kwa ngazi ya stashahada, hasa kwa wanafunzi wa masomo ya sayansi na ufundi, huku ikiongeza kiwango cha fedha za kujikimu kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

Katika kukuza vipaji na kuandaa wataalamu wa siku zijazo, Waziri ameeleza kuwa mpango wa Samia Scholarship umefadhili wanafunzi 1,343 wanaosomea masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM). Uwekezaji huo umeungwa mkono na uanzishwaji wa vyuo 93 vya VETA, pamoja na vituo vya umahiri kama DIT, ATC, na NIT kupitia mradi wa EATSTRIP, sambamba na kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha TEHAMA Zanzibar.

Amesema mafanikio hayo yamechagizwa na uwekezaji mkubwa katika walimu na miundombinu ya kufundishia.

Licha ya hayo Serikali imetoa mafunzo kazini kwa zaidi ya walimu 250,000, huku vyuo vya ualimu vikiunganishwa na Mkongo wa Taifa. Pia, wizara imeongoza matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa taasisi za elimu, hatua inayochangia mazingira bora ya kufundisha na kujifunzia.

Katika hatua nyingine, Prof. Mkenda amesema zaidi ya vyumba vya madarasa 50,000 vimejengwa au kuboreshwa katika shule za msingi na sekondari nchini ambapo Serikali imejenga shule mpya za sekondari za wasichana zinazolenga masomo ya sayansi, pamoja na shule maalum na za elimu jumuishi, hatua iliyowezesha ongezeko kubwa la wanafunzi wenye mahitaji maalum kupata elimu.

“Mafanikio haya yote yanaakisi maono ya Rais Samia ya kujenga taifa lenye rasilimali watu iliyoelimika, yenye ujuzi na inayoweza kushindana duniani,Elimu na ujuzi ndio msingi wa maendeleo endelevu ya taifa letu,” amesisitiza.