Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeanza rasmi utekelezaji wa mpango mkubwa wa kubadilisha sura ya eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam kwa kuvunja majengo yote chakavu na kujenga majengo ya kisasa yanayokidhi mahitaji ya sasa ya makazi, biashara na huduma nyingine za mijini.

Akizungumza leo katika kikao na Jukwaa la Wahariri Tanzania, TEF Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdalah, amesema mageuzi hayo yatafanyika ndani ya kipindi cha miaka mitatu, yakihusisha kuvunjwa kwa jumla ya majengo 64 yaliyopo chini ya Shirika hilo.

“Hakutakuwa tena na jengo chakavu la NHC katika Kariakoo ndani ya miaka mitatu. Tayari tumeanza na miradi 16 ambapo majengo ya zamani yamevunjwa na ujenzi wa mapya unaendelea,” alisema Hamad.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, majengo hayo mapya yataanzia ghorofa 10 na kuendelea, yakichanganya matumizi ya makazi, biashara, huduma za kijamii na ofisi. Aidha, miradi hiyo inatekelezwa kwa mfumo wa ubia na sekta binafsi pamoja na ujenzi unaofanywa moja kwa moja na Shirika lenyewe.

“Ni muda wa kufanya matumizi bora ya ardhi, hasa katika maeneo ya kibiashara kama Kariakoo. Kila kipande cha ardhi tunachomiliki kitumike kwa tija kiuchumi na kijamii,” alisisitiza.

Mradi huu ni sehemu ya mkakati mpana wa NHC wa kuimarisha uwekezaji katika maeneo ya kimkakati nchini, hasa mijini, kwa lengo la kuboresha muonekano wa miji, kuhimiza uwekezaji na kuinua sekta ya ujenzi na makazi.

Hamad alibainisha kuwa Shirika hilo linaendelea kusimamia miradi yake kwa uwazi na weledi, likishirikiana kwa karibu na vyombo vya habari ili kuhakikisha umma unapata taarifa sahihi kwa wakati.

“Hili si suala la ujenzi pekee, bali ni mageuzi ya fikra kuhusu matumizi ya ardhi, ujenzi wa miji na msingi wa maendeleo endelevu kwa vizazi vijavyo,” alisema kwa msisitizo.

Kikao hicho na Jukwaa la Wahariri kilikuwa sehemu ya ziara ya kutembelea miradi mbalimbali ya NHC ikiwemo Kawe 711, GPR Kawe, Samia Housing Scheme na Morocco Square, ambapo wahariri walipata fursa ya kujionea maendeleo na ubora wa miradi hiyo.