Na Zulfa Mfinanga, JamhuriMedia,
Arusha.
Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, iliyoko Arusha, imetoa hukumu ya kihistoria katika kesi ya Tembo Hussein dhidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikibatilisha hukumu ya kifo na kutangaza kuwa adhabu hiyo ni kinyume cha haki za binadamu.
Tembo Hussein ambaye alikuwa akisubiri kunyongwa katika Gereza Kuu la Uyui mkoani Tabora, alifungua kesi dhidi ya Serikali ya Tanzania akidai ukiukwaji wa haki zake wakati wa kesi ya mauaji iliyompelekea kuhukumiwa kifo.
Katika utetezi wake Tanzania ilidai kuwa Mahakama haina mamlaka ya kuingilia maamuzi ya Mahakama zake za juu lakini Mahakama ya Afrika ilibainisha kuwa inaweza kuingilia iwapo haki za msingi zimekiukwa.
Mahakama ilifafanua kuwa haitekelezi kazi za mahakama ya rufaa bali hutathmini iwapo haki za binadamu zimeheshimiwa kulingana na mikataba ya kimataifa.
Katika hukumu hiyo Mahakama ilitupilia mbali pingamizi la Tanzania kuhusu mamlaka yake na ikasisitiza kuwa ipo ndani ya uwezo wake kutoa maagizo kama kuachiliwa kwa mfungwa ikiwa haki zake zilikiukwa.
Mahakama ilithibitisha kuwa Tembo Hussein alifuata taratibu zote za kisheria zilizopo nchini Tanzania kabla ya kufika katika Mahakama hii ya Afrika na hivyo shauri lake lilikuwa halali kisheria.
Licha ya madai kuwa hakupata haki ya kusikilizwa mbele ya mahakama isiyo na upendeleo, Mahakama ilikosa ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa maafisa wa mahakama walionyesha upendeleo au walivuruga ushahidi.
Hata hivyo Mahakama ilitilia mkazo kuwa Tembo Hussein alihukumiwa chini ya sheria inayotamka adhabu ya kifo kama ya lazima jambo ambalo linakiuka haki ya msingi ya kuishi na utu wa binadamu.
Mahakama hiyo ilieleza kuwa kutomruhusu jaji kuzingatia mazingira ya kosa na hali ya mtuhumiwa kabla ya kutoa hukumu ya kifo ni ukandamizaji wa haki ya binadamu.
Aidha Mahakama iliamua kuwa njia ya utekelezaji wa adhabu ya kifo kwa kunyongwa ni adhabu ya kikatili na ya kinyama hivyo inakiuka Kifungu cha 5 cha Mkataba wa Haki za Binadamu.
Kwa kuzingatia haya Mahakama iliagiza Serikali ya Tanzania ifute hukumu ya kifo dhidi ya Tembo Hussein na kumtoa kwenye orodha ya wanaosubiri kunyongwa, akisubiri kesi yake isikilizwe upya.
Aidha Mahakama iliiamuru Serikali ya Tanzania kufanya mabadiliko ya kisheria ndani ya miezi sita kwa kuondoa adhabu ya lazima ya kifo kutoka kwenye sheria zake.
Pia ilielekeza adhabu ya kunyongwa iondolewe kama njia ya utekelezaji wa hukumu za kifo huku Serikali ikiagizwa kuripoti utekelezaji wa maagizo hayo kila baada ya miezi sita.
Mahakama iliamuru hukumu hii ichapishwe kwenye tovuti ya Mahakama, Wizara ya Katiba na Sheria, na kuhifadhiwa kwa mwaka mmoja kwa matumizi ya umma.
Mahakama haikutaja fidia ya kifedha lakini ilibainisha kuwa kila upande ubebe gharama zake na kuonyesha kuwa kesi hii ilikuwa zaidi kuhusu haki na mabadiliko ya mfumo.
Kesi kama hii zimekuwa zikiibua mijadala mikubwa kuhusu adhabu ya kifo barani Afrika huku wito ukiendelea kutolewa kwa mataifa mengine kutathmini upya sheria zao ili kuendana na viwango vya haki za binadamu vya kimataifa.
