Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), Innocent Lugha Bashungwa, ametangaza rasmi nia ya kuendelea kulihudumia Taifa kupitia nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Karagwe kwa kuchukua na kurejesha fomu ya kugombea kupitia CCM.
Tukio hilo limefanyika katika Ofisi za Chama Wilaya ya Karagwe, ambapo fomu hiyo imepokelewa na Katibu wa CCM Wilaya ya Karagwe, Ndugu Anatory Nshange, huku likishuhudiwa na makada, wanachama wa chama hicho, na wananchi waliokusanyika kwa hamasa.
Bashungwa amekuwa Mbunge wa Jimbo hilo kwa vipindi viwili mfululizo tangu mwaka 2015 hadi sasa, na katika kipindi hicho ameaminiwa kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, ikiwemo kuwa Naibu Waziri wa Kilimo; Waziri wa Viwanda na Biashara; Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo; Waziri wa TAMISEMI; Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa; Waziri wa Ujenzi; na kwa sasa ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Kwa mujibu wa Bashungwa, hatua yake ya kuomba tena ridhaa ya wananchi inalenga kuendeleza kazi ya maendeleo aliyoianzisha pamoja na kuimarisha mshikamano, utawala bora na uwajibikaji kwa maslahi ya wananchi wa Karagwe.
“Nimerudi nyumbani tena kuomba dhamira yenu. Karagwe ni nyumbani, na maendeleo yetu ni dhamira ya moyo wangu,” alisema Bashungwa.
Hatua yake ya kuchukua fomu inaashiria mwanzo wa mchuano mkali wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, huku wananchi wakisubiri kwa hamu kuona mustakabali wa uongozi wa jimbo hilo.

