Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
TAASISI ya Uhasibu Tanzania (TIA), imeandaa mkutano mkubwa wa kitaaluma utakaofanyika hivi karibuni mkoani Mwanza wenye lengo la kuelezea tafiti mbalimbali zilizofanywa na wataalamu wa taasisi hiyo.
Kadhalika, imesema imeendelea kufungua kampasi kwenye mikoa mbali mbali kama sehemu ya kuwa karibu zaidi na wananchi wanaotaka kunufaika na elimu wanayotoa.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Ofisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Profesa William Palangyo, kwenye Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa maarufu kama sabasaba.

Alisema TIA imekuwa ikifanya mikutano kama hiyo kila mwaka kwa lengo la kusogeza taaluma inayotolewa na taasisi hiyo iwafikie wananchi waliowengi.
Alisema mkutano huo umekuwa ukisaidia kuwasilisha tafiti mbalimbali zinazofanywa na wataalamu wa taasisi hiyo ili waweze kuzitumia kwa manufaa yao katika maeneo ya uhasibu, manunuzi na maeneo ya kiutawala na uongozi.
Alisema mkutano huo utawashirikisha wanataaluma wa fani ya uhasibu na manunuzi kutoka vyuo mbalimbali nchini ambao watatoa mada kwenye mkutano.

Alisema katika kuendelea kupanua wigo wa elimu inayotolewa na taasisi hiyo wameanzisha Shahada mpya ya mambo ya biashara na shahada ya uchumi na fedha.
Alisema pia wanatarajia kuanzisha Shahada ya Uzamili katika fani ya monitoring and evaluation ambayo ni mpya kufundishwa kwenye taasisi hiyo.
“Na TIA tunazidi kusogea karibu na wananchi tulikuwa na kampasi saba sasa tunayo ya nane ya mkoani Tanga kwaajili ya watu wa kaskazini ambao wangependa kupata elimu inayotolewa na taasisi yetu,” alisema.
Alisema ili kuhakikisha wananchi wengi wananufaika na elimu inayotoa TIA mbali na kampasi ya Dar es Salaam ilifungua matawi mengine katika mikoa ya Singida, Mbeya, Mtwara, Mwanza, Kigoma, Zanzibar na Tanga.

Profesa Palangyo alisema TIA imeanzisha pia taasisi inayosimamia masuala ya ushauri wa kitaalamu inayoitwa Tanzania Institute of Accountancy Consultancy Burearu ambayo iko kwaajili ya kutoa ushauri wa kitaalamu.
“Taasisi hii inasaidia kutoa ushauri pale mtu anapokuwa na changamoto yoyote ya biashara na kwenye fani ambazo tumebobea kama uhasibu na masuala ya manunuzi na watu wengi wamenufaika nayo,” alisema
“TIA inaendelea kukua na kwa sasa inachukua zaidi ya wanafunzi 30,000 na tumehakikisha kila mwaka tunaendelea kuwa karibu na wananchi ili waweze kunufaika na elimu yetu,” alisema
Alisema kuna idadi kubwa ya wanafunzi wanaohitimu elimu ya msingi na kwenda kwa wingi sekondari hali ambayo alisema imesababisha mahitaji makubwa ya elimu ya vyuo vikuu na vya kati.

Alisema kwa kuzingatia mahitaji hayo, TIA imeendelea kupanua miundombinu yake ili kuiwezesha kuchukua idadi kubwa ya wanafunzi wanaohitimu sekondari kila mwaka.
Alisema kwa kuanzia mwaka jana na mwaka huu wanaendelea na miradi ya ujenzi wa majengo ya wanafunzi yenye thamani ya shilingi bilioni 59.2 kwenye kampasi zake.
Alisema ujenzi huo unalenga kuhakikisha wanafunzi wanaojiunga na taasisi hiyo wanapata maeneo mazuri ya kusomea, vyumba vya kompyuta na maktaba.

