Israel na kundi la Hamas linalotawala Ukanda wa Gaza zimechukua msimamo tofauti leo kuhusiana na pendekezo la Rais Donald Trump wa Marekani la usitishaji mapigano kwa muda wa siku 60.

Saa kadhaa baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kutangaza kuwa Israel imeridhia masharti ya usitishaji vita vya Gaza kwa siku 60 na kulirai kundi la Hamas nalo likubali pendekezo hilo, pande hizo mbili hasimu zimechukua msimamo tofauti.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Israel Gideon Saara, ameonesha kuunga mkono tangazo la Trump akisema utawala mjini Tel Aviv “unaikaribisha kwa mikono miwili nafasi yoyote” itayowezesha kuachiwa huru kwa mareka wa Israel wanaoshikiliwa Gaza.

Kupitia ujumbe katika mtandao wa kijamii wa X, mwanadiplomasia huyo amesema fursa ya aina hiyo “haiwezi kuachwa ipite” na hilo linaungwa pia mkono na idadi kubwa ya watu nchini Israel.

Katika tangazo lake la jana kwenye mtandao wa Truth Social, Rais Trump alisema Israel imekubali masharti ya pendekezo la usitishaji vita kwa muda wa siku 60.

Trump amesema anataraji usitishaji mapigano kwa miezi hiyo miwili utaanza mapema wiki ijayo na amelitaka kundi la Hamas likubali pendekezo hilo akionya kuwa “hali itazidi kuwa mbaya” iwapo italikataa.

Amesema siku hizo 60 zitatumika kutafuta njia ya kuvimaliza vita vya Gaza jambo ambalo Israel imekuwa ikilipinga, ikisema haitositisha vita hadi pale kundi la Hamas litakapotokomezwa kabisa.