MSANII mashuhuri wa muziki wa hip-hop, Sean Diddy Combs maarufu kama P Diddy, ameendelea kusalia rumande baada ya Jaji Arun Subramanian wa Mahakama ya Shirikisho kumkatalia dhamana, licha ya kupunguziwa baadhi ya mashtaka.

Combs alikutwa na hatia ya kujihusisha na biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu na ukahaba, huku mashtaka mazito ya ulaghai na biashara ya ngono yakiondolewa. Hukumu kamili ya kesi hiyo imepangwa kutolewa Oktoba 3 mwaka huu, ambapo anatarajiwa kukabiliwa na kifungo cha hadi miaka 20 jela.

Mawakili wake walijaribu kumshawishi jaji kwa kueleza kuwa hana hatari ya kutoroka, wakidai ndege anayotumia inakodishwa Hawaii.Hata hivyo, Jaji Subramanian alikataa ombi hilo kutokana na historia ya unyanyasaji inayomkabili msanii huyo.

Katika kesi hiyo iliyodumu kwa takriban miezi miwili jijini New York, waendesha mashtaka walieleza kuwa Combs alitumia umaarufu wake na ushawishi wa kibiashara kuwaendesha wanawake kwa ajili ya biashara ya ngono, hali iliyotajwa kuwa sehemu ya mtandao wa kihalifu.

Kwa sasa, Combs ataendelea kuzuiliwa katika gereza la shirikisho lililopo Brooklyn, ambako amekuwa kizuizini tangu Septemba mwaka jana akisubiri hukumu ya mwisho.