Na Mwandishi Wetu, Mtwara

Chama cha Wananchi (CUF) kimesema hakitasusia uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025 badala yake kitashiriki kikamilifu zoezi hilo.

Hayo yalibainishwa wakati wa mkutano wa hadhara wa kitaifa wa chama hicho Jimbo la Mtwara Mjini uliyofanyika Manispaa ya Mtwara Mikindani, Mtwara.

Akizungumza katika mkutano huo wa hadhara, Makamu Mwenyekiti wa CUF Taifa Othman Omar Dunga alisema wananchi wa chama hicho wasisusie uchaguzi huo badala yake wahakikishe wanaichagua CUF kama walivyoichagua uchaguzi wa mwaka 2015.

“Tunaona faida na hasara ya kususia uchaguzi na kwamba hasara ni kubwa kuliko kususa uchaguzi, tunawaambia wananchi wa Mtwara msisusie uchaguzi, hakikisheni mnakichagua chama cha CUF kama mlivyotuchagua mwaka 2015″alisema Dunga.

Aliongeza kuwa, “Hakikisheni kwa umoja wenu na bila kugawanywa kama hivi mnavyogawika, msifate mtu fateni chama chenu hiki ambacho mlikuwa nacho”

Alisema chama hicho kipo mstari wa mbele kuhakikisha kwamba wanatetea haki na uhuru wa mtanzania huku kikiahidi kuwa kitaendesha mchakato wa kampeni za kistaarabu na za kiungwana wanapoelekea katika uchaguzi huo.

Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki na Kati kwa tiketi ya CUF, Mashaka Ngole aliwasisitiza wanachama wa chama hicho kushiriki kikamilifu zoezi hilo la uchaguzi kwasababu ni haki yao ya msingi.

Katika hatua nyingine chama hicho kimeweka mawe ya msingi katika baadhi ya maeneo kwenye jimbo hilo ikiwemo eneo la ujenzi wa ofisi ya chama kata ya magomeni kwenye manispaa hiyo.