Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia,Dodoma
Sekta ya madini imeendelea kuwa kichocheo kipya cha maendeleo kwa Mkoa wa Tanga, ambapo wananchi katika maeneo mbalimbali wameanza kunufaika na shughuli za utafutaji, uchimbaji na biashara ya madini.
Kupitia usimamizi madhubuti wa Serikali ya Awamu ya Sita, sekta hii imesaidia kuhamasisha uwekezaji, kuongeza ajira na kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Salha Burian, ameeleza hayo leo July 15 ,2025 Jijini hapa kwenye mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu mafanikio yaliyopatika kwenye mkoa huo kwa kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya Sita.
Amesema kuwa ongezeko la wachimbaji wadogo na masoko ya madini yaliyosajiliwa limeongeza uwazi na tija katika sekta hiyo, huku wilaya za Handeni, Kilindi na Korogwe zikitajwa kuwa vinara wa mafanikio hayo.
Mbali na madini amesema Mkoa wa Tanga umetekeleza kwa mafanikio makubwa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF), ambapo jumla ya walengwa 38,952 sawa na asilimia 57 wameanzisha biashara ndogo ndogo kama mama lishe, uuzaji wa kuku na samaki.
Aidha ameeleza kuwa zaidi ya walengwa 48,645 (asilimia 71) wameweza kujiunga na Bima ya Afya (CHF), hali iliyosaidia kuwawezesha kupata huduma za afya kwa wakati.
“Pia, kaya 44,234 zimeweza kuanzisha shughuli za kilimo na ufugaji wa kuku, mbuzi, ng’ombe na kondoo kwa mafanikio makubwa, ” amesema.
Katika kuimarisha mazingira ya kiuchumi kwa wananchi wake,Dkt.Burian amesema Mkoa wa Tanga umeendelea na utekelezaji wa miradi mikakati inayolenga kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na Mkoa kwa ujumla.
Ameitaja Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa Jengo la Biashara la Dkt. Samia Suluhu Hassan Business Centre linalowalenga wafanyabiashara, ujenzi wa soko la kisasa la machinga, pamoja na ujenzi wa Kituo cha Michezo cha TFF katika eneo la Mnyanjani kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 4.5, ambacho kinalenga kukuza vipaji vya vijana.

Amefafanua kuwa Mradi mkubwa wa kimkakati unaoendelea kwa kasi katika Mkoa wa Tanga ni ule wa ujenzi wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanga.
” Bomba hili lenye urefu wa kilomita 205.91 limekamilika kwa asilimia 53 huku shughuli za fidia kwa wananchi waliopisha mradi huo zikifikia asilimia 98.7,Wananchi 1,560 kati ya 1,580 tayari wamelipwa jumla ya shilingi bilioni 9.38, na wengine 40 wamejengewa nyumba 43 mbadala ambazo zimekamilika kwa asilimia 100,”ameeleza
Amesema Mradi huo pia umezalisha ajira zaidi ya 810 katika eneo la Chongoleani, sambamba na kuibua fursa nyingine za biashara kama mama lishe, huduma za usafiri, na huduma ndogo za kifedha.
Amesema Bandari ya Tanga pia imepewa msukumo mpya kupitia mradi wa maboresho uliofanywa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa gharama ya shilingi bilioni 429.1 na kwamba Maboresho hayo yameongeza ufanisi wa bandari hiyo ambapo muda wa kuhudumia meli umepungua kutoka siku 5 hadi siku 2.
” Idadi ya meli zilizohudumiwa imeongezeka kutoka meli 198 mwaka 2021 hadi meli 307 mwaka 2025, huku shehena ya mizigo ikipanda kutoka tani 888,130 hadi tani 1,191,480,makasha yanayopakiwa na kupakuliwa yameongezeka kutoka TEUs 7,036 hadi TEUs 7,817,hii imesababisha ongezeko la mapato na ajira za muda mrefu na muda mfupi kwa wakazi wa Tanga, “amesema.
Amesema Mkoa wa Tanga umepokea zaidi ya shilingi bilioni 1.1 kwa ajili ya ukarabati mkubwa wa kivuko cha MV Tanga ambacho ni mkombozi mkubwa kwa wananchi wanaotegemea usafiri wa majini ambapo Kivuko hicho kinatarajiwa kurahisisha huduma za usafirishaji na kukuza biashara kati ya maeneo ya mwambao na bara.
Katika kuimarisha utawala bora, Mkuu huyo wa Mkoa wa Tanga amesema, Mkoa huo umeendelea kutekeleza misingi ya uwajibikaji na uwazi kwa kuanzisha Kamati za Uadilifu katika kila taasisi ya umma, kusikiliza kero za wananchi kwa wakati na kuhakikisha zinafanyiwa kazi.
“Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) inaendelea na kazi ya kuokoa mali na rasilimali za umma kwa kuzibaini mapema na kuchukua hatua dhidi ya wahusika wasio waaminifu,kuongezeka kwa idadi ya mahakama za mwanzo kutoka 65 mwaka 2020 hadi 67 mwaka 2025 na Wilaya kutoka 6 hadi 8, ni kielelezo cha jitihada za kupeleka huduma za haki karibu na wananchi, “amesema