

…………………
.Hotuba ya Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo Ndg. Dorothy Jonas Semu kwa Halmashauri Kuu tarehe 23 Februari, 2025
Ndugu Mwenyekiti wa Chama
Ndugu Makamu Mwenyekiti Bara
Ndugu Makamu Mwenyekiti Zanzibar
Ndugu Viongozi, wajumbe wa Halmashauri Kuu na Kamati Kuu
Ndugu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamiini
Ndugu wanachama na wageni
Ndugu wanahabari
Kwanza kabisa napenda kuwakaribisha katika Mkutano huu wa Halmashauri Kuu ya kwanza muhimu ya mwaka 2025. Ni kikao na muda muhimu wa kujadili masuala muhimu kwa ajili ya mafanikio ya chama chetu na jamii ya watanzania na hasa ukizingatia kuwa mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu.
Niwapongeze kutambua mchango wa wanachama na viongozi wetu katika ujenzi wa chama, chama kinachobeba matumaini ya watanzania. Mchango mkubwa wa utendaji hali na mali kufanikisha ushiriki wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024. Mchango wenu umekuwa wa thamani kubwa katika kuhakikisha tunafikia malengo yetu.
Hata hivyo, ninaendelea kuweka bayana hali tuliyonayo sasa katika kufikia demokrasia ya nchi yetu tukichukua uzoefu wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019, Uchaguzi Mkuu 2020, Uchaguzi wa Serikali za mitaa 2024, imetudhihirishia kwamba;
Chama cha Mapinduzi hakitaki na hakiwezi kushindana kwenye uchaguzi wa haki, huru na wa kuaminika.
Uchaguzi unatawaliwa na mabavu ikiwemo vipigo, kamatakamata, utekaji na mauaji ya wanachama na wananchi wanaopinga wizi wa kura.
Chaguzi zilitawaliwa na mbinu mbalimbali hasa matumizi ya makubwa ya kura haramu.
Viongozi, wanachama na wananchi wanaendelea kupoteza matumaini kutokana na mwenendo usioridhisha wa chaguzi zetu.
Vyombo vya dola ikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama na mifumo yote ya kiserikali vinakipendelea Chama cha Mapinduzi (CCM)
Ni vizuri kukumbushana kuwa pamoja na hayo yote uchaguzi ni kama VITA.
Vita ina majira yake. Kuna wakati wa faraja ya ushindi na kuna wakati wa majanga katika vita (casualities).
Kuna wakati wa ari ya kimapambano kutokana na dalili ya ushindi au ushindi kwenye baadhi ya mapambano na kuna kipindi cha kuvunjika ari kutokana na kupoteza baadhi ya mapambano (battles).
Wajibu wa jemedari mzuri ni kutambua hali halisi katika vita na kuchukua hatua stahiki. Jemedari hapaswi kukata tamaa, bali anapaswa kuchukua hatua stahiki kulingana na hali halisi.
Chama chetu kipo katika hali ya vita inayotokana na mazingira yanayokatisha tamaa. Wajibu wetu kama majemedari katika vita yetu ni kuhakikisha kuwa hatukati tamaa. Iwapo Wajumbe wa Halmashauri Kuu tutakata tamaa, hilo litakuwa ni tamko la kushindwa vita, jambo ambalo hatuwezi kuliruhusu kutokea.
Bila shaka kila mmoja wetu aliingia kwenye mapambano haya akijua kuwa hayatakuwa rahisi. Chama chetu kinapaswa kujipanga vizuri kuhakikisha kuwa tunadhibiti hujuma za CCM na dola na tunafanikisha malengo yetu ya kisiasa kama ambavyo majemedari hodari kwenye vita mbalimbali ulimwenguni waliweza kuusoma mwelekeo wa vita, kufufua ari ya mapambano na kusonga mbele hadi kuupata ushindi.
Kwa mshikamano wetu, kwa hakika, tutayafikia malengo yetu. Ndugu zangu, ni wakati wa kuchukua hatua. Tuwe na mshikamano na umoja katika kukabiliana na matatizo yanayotukabili. Kwa pamoja, tunaweza kufanikisha malengo yetu na kuleta mabadiliko tunayoyahitaji.
Tukielekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, ni muhimu kutambua kwamba kuna hujuma na hila zinazotumiwa ili kukata tamaa wananchi. Hali hii inatufanya tuwe na jukumu kubwa la kusukuma ajenda ya kuunda jukwaa la mapambano ya pamoja na vyama makini. Tunahitaji kufanya shughuli za pamoja ili kuimarisha umoja wetu wenye nguvu utakao leta tija ya mabadiliko.
Tunahitaji kupambania kuurejesha uchaguzi. Nchi yetu hasa hakuna uchaguzi, tuna uchafuzi. Tutaunganisha nguvu na vyama vyote makini na wadau wa demokrasia nchi.
Pamoja na hayo yote bado tunashuhudia matatizo makubwa ya wananchi kutokana kushindwa kwa Serikali ya CCM. Tukiendelea kuiacha CCM tena hali itakuwa mbaya zaidi.
Kiuchumi kwa miaka minne ya Rais Samia tunaona wimbi kubwa la uporaji wa rasilimali za nchi yetu kwa jina la uwekezaji usiojali maisha ya wanannchi wa kawaida.
Tumeshuhudia ardhi ikiendelea kuporwa na wananchi wakiendelea kutaabika Ngorongoro, Mbarali, Kilosa na Kasulu.
Mikataba kama vile bandari, gesi, bado inafanywa gizani na wananchi hawana taarifa ya nini kinachoendelea mfano; majuzi tumesikia suala la makubaliano kuhusiana na uendeshaji wa bandari ya Bagamoyo na hakuna mijadala yoyote katika vyombo vya uwakilishi ndani ya nchi badala yake tunasikia katika vyombo vya serikali ya nchi nyingine. Hata ukanusho wa serikali haujaweka bayana nini inachoendelea katika uwekezaji wa bandari ya Bagamoyo usiri, usiri, usiri!
Huduma za jamii: Afya imeendaelea kuwa mwiba kwa wananchi wengi nchini. Gharama zimeendelea kuwa juu na serikali haina ufumbuzi wa suala hili badala yake imeendeleza vifurushi vya kuuza huduma ya afya ikiwatenga wananchi masikini.
Ajira: Ajira bado ni changamoto kubwa, juzi mmesikia vijana wahitimu wa kada ya ualimu wakieleza masikitiko yao makubwa kuhusu ajira ya ualimu nchini.
Serikali inapiga propaganda kwamba hakuna uhaba wa walimu lakini takwimu zinaonyesha uhitaji wa walimu ni 279,202 kwa shule za msingi na sekondari.
Wakati walimu waliopo mtaani ni 146,000 kwa hiyo hata serikali ikiajiri vijana walimu wanaosota mtaani bado kutakuwa na mahitai makubwa ya walimu nchini. Hali ni hivyo hivyo kwenye sekta ya afya, kilimo ambazo ni sekta muhimu katika kuimarisha nguvu kazi ya Tanzania.
Ndugu Viongozi na Wajumbe wa Halmashauri Kuu jitihada zozote za kufanya mageuzi ya siasa ili kupata viongozi wanaojali hali ya wananchi wetu ni jitahada za kufa na kupona.
Tunahitaji kuibeba vita hii ya kupigania mageuzi ili kuleta ustawi bora wa watu wetu. Tunapaswa kuunganisha nguvu za wapenda Demokrasia, wananachi na makundi mingine dhidi na wapuuza demokrasia.
Ni wito wangu kwenu kuelewa kuwa kazi hii inapaswa kufanywa kwa gharama zozote. Tunapaswa kuwa tayari kulipia gharama za mapambano haya.
Mimi, Kiongozi wenu ninawahakikishia kuwa nipo tayari kuongoza mapambano dhidi ya wadhalimu, wapinga demokrasia na vyombo vyao vya mabavu na nipo tayari kulipa gharama ya mapambano hayo kwa maslahi ya taifa letu na kwa maslahi ya wananchi waliotuamini.
Na viongozi wote tuliopo hapa, tumejiandaa kwa hilo. Je, wajumbe wa Halmashauri Kuu mpo tayari kwa mapambano? Mpo tayari kulipa gharama yoyote ya mapambano yetu?
Mungu ibari Tanzania, Mungu abariki dhamiri zetu. Mungu awajaze ujasiri zaidi ya kukabiliana na wapinga demokrasia nchini.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.








