Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,
Mara

JESHI la Polisi Mkoa wa Mara linamshikilia Samweli Emmanuel maarufu kwa jina la ‘Nzaliya’ (20), mkazi wa kijiji cha Nata, Wilaya ya Serengeti, kwa tuhuma za mauaji ya Josephina Magani (52), ambaye pia ni mkazi wa eneo hilo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Polisi Mei 8,2025 imeeleza kuwa tukio hilo lilitokea Mei 7, 2025, majira ya saa 1, usiku katika kitongoji cha Mambaswe, kijiji cha Nata. Kwa mujibu wa taarifa za polisi, inadaiwa kwamba Samweli alimshambulia Josephina kwa kutumia kisu, akimchoma tumboni na kusababisha upotevu mkubwa wa damu uliompelekea marehemu kufariki dunia papo hapo.

Aidha baada ya mauaji hayo, imedaiwa mtuhumiwa aliburuta mwili wa marehemu kutoka nyumbani kwake na kuuficha kwenye shimo ambalo awali lilitumika kwa shughuli za uchimbaji madini ya dhahabu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba chanzo cha tukio hili ni ugomvi wa kifamilia, ambapo mtuhumiwa alikuwa akimshutumu marehemu kwa kumuabukiza virusi vya ugonjwa wa UKIMWI ambapo awali walikuwa wakiishi kama mume na mke.

Jeshi la Polisi limewaasa wananchi waendelee kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa za uhalifu badala ya kujichukulia sheria mkononi, ili kuhakikisha haki inapatikana na wahalifu wanakabiliwa ipasavyo kisheria.