Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imewataka Watanzania kujitokeza katika msimu wa Tamasha la utamaduni la Afrika ya kusini litakalofanyika kwa wiki moja.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Said Yakubu amesema tamasha hilo litaambatana na matukio mbalimbali ikiwemo tamasha la muziki,maonyesho ya mavazi, ngoma za asili ikiwa ni pamoja kutembelea maeneo ya kihistoria katika ya Tanzania na Afrika ya kusini yalipo nchini.

”Leo jioni kutakuwa na ufunguzi wa rasmi wa tamasha hili katika ukumbi wa Mlimani city na Waziri Mchengerwa atakuwepo,watu zaidi ya 1000 wanatarajiwa kuhudhuria lakini pia tamasha hili litafanyika katika maeneo mbalimbali ” Alisema Yakubu

Aidha amesema tamasha hilo linafaida kubwa kwa wasanii mbalimbali kwani watapata fursa ya kuonesha kazi zao za sanaa,kujifunza na kubadilishana uzoefu na wageni .

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Afrika ya Kusini Nocawe Mafu amesema tamasha hilo linalenga kukuza uhusiano wa Tanzania na Afrika ya Kusini,kudumisha na kukuza utamadani na kubadilishana uzoefu.

” Nchi hii kwetu sisi ni kama nyumbani kwetu,Afrika kusini na Tanzania ina uhusiano wa kihistoria tokea zamani,Mwalimu Julius Nyerere alipigana kwa hali na mali kuhakikisha Afrika Kusini inapata uhuru wake” amesema Mafu.

Ameongeza kuwa licha ya burudani zitakazotolewa kwenye msimu wa tamasha hilo kutakuwa na semina ya biashara ya kazi za sanaa ikiwemo muziki, maonyesho ya filamu,maonesho ya picha za kuchora kutoka Afrika ya kusini.

“Tunategemea tamasha hili litaimarisha mahusiano yetu,baina ya nchi zote mbili na watu wake, kufanya utalii,kukuza diplomasia,wasanii kupata uzoefu na fursa mpya pamoja na kukuza uwelewa wa sanaa biashara “ amesema.

Please follow and like us:
Pin Share