Na Zulfa Mfinanga, JamhuriMedia, Arusha.
Baraza la Huru la Habari Afrika (NIMCA) limepitisha maazimio yatakayobadilisha sura ya uandishi wa habari katika bara hilo.
Katika kilele cha Mkutano huo baraza limeweka msingi wa mageuzi kupitia matumizi sahihi ya teknolojia ya akili bandia (AI), ujumuishaji wa makundi yaliyotengwa na uimarishaji wa ushirikiano wa kimkakati kati ya serikali, taasisi za elimu na sekta binafsi.
Baraza hilo limeamua kuandaa miongozo maalum ya matumizi ya AI kwa vyumba vya habari kwa lengo la kuhakikisha uadilifu na maadili katika uundaji wa maudhui.
AI imeonekana si tishio kwa wanahabari bali ni mshirika wa karibu katika kusukuma mbele taaluma ya habari.
Katika kuhakikisha kuwa kila mmoja anapata nafasi katika tasnia ya habari baraza limetoa wito kwa vyombo vya habari kuhuisha sera zao za ujumuishaji hasa kwa kuzingatia jinsia na watu wenye ulemavu huku mafunzo ya kuripoti masuala ya watu wenye ulemavu yakipewa kipaumbele.

Serikali na wizara husika zimehimizwa kuandaa sera thabiti za kitaifa kuhusu AI zenye malengo ya muda mrefu ili mataifa ya Afrika yajiandae kikamilifu kwa mapinduzi ya kidijitali yanayoendelea kushika kasi duniani.
Kwa kutambua umuhimu wa elimu mkutano huo umeazimia kuingiza masuala ya teknolojia shirikishi katika mitaala ya shule huku vituo vya ubunifu vikiwekewa mazingira rafiki ya kufanikisha mawazo yanayochipua kutoka kwa vijana wa Kiafrika.
Sera za uelewa wa kidijitali na matumizi ya vyombo vya habari kwa manufaa ya wananchi zimeelezwa kuwa nguzo muhimu za maendeleo huku serikali zikihimizwa kuziboresha sheria za habari ili kuwezesha mazingira salama na huru kwa wanahabari.
Katika juhudi za kuhifadhi utamaduni wa Kiafrika mkutano umehimiza uundaji wa mifumo ya AI inayotambua lugha na hadithi za asili pamoja na kuwekeza kwenye hifadhidata za kidijitali zitakazosaidia kulinda urithi wa bara hili.
Miundombinu ya habari kama TEHAMA, huduma za intaneti zenye kasi na vifaa vya kidijitali mashuleni imepangwa kuwa mojawapo ya maeneo yatakayowekewa kipaumbele kwa uwekezaji wa haraka.
Baraza limeazimia kuanzisha ushirikiano wa mataifa ya Afrika katika kuweka sera za haki kwa majukwaa ya kidijitali kuhakikisha kuwa wachapishaji wa habari wananufaika kiuchumi kwa kazi zao.

Katika kipengele cha udhibiti na umiliki maazimio yanasisitiza uhitaji wa mbinu bunifu za ufadhili endelevu ili vyombo vya habari viweze kufanya kazi kwa uhuru bila utegemezi wa kisiasa au wa kibiashara usio na tija.
NIMCA imepewa jukumu muhimu la kuanzisha hifadhi ya kidijitali ya urithi wa Afrika na kuweka mfumo wa pamoja wa kushughulikia malalamiko dhidi ya vyombo vya habari ili kuongeza uwazi na uwajibikaji katika sekta hiyo.
Baraza pia limeitaka NIMCA kufuatilia utekelezaji wa sera zinazohusiana na ujumuishaji ndani ya vyombo vya habari kuhakikisha kuwa sauti zote katika jamii zinapata nafasi sawa kusikika.
Taasisi za elimu zimepewa wajibu wa kufanya mapitio ya mara kwa mara ya mitaala yao ili kuhakikisha zinawajengea wanafunzi maarifa na maadili ya kutumia AI kwa ufanisi katika uandishi wa habari.
Pia baraza limehimiza vyuo vikuu kufanya tafiti zinazojikita katika mazingira halisi ya Afrika kwa lengo la kuunda maarifa mapya yatakayosaidia kuboresha tasnia ya habari kwa vizazi vijavyo.