Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Fatuma Mwasa, amezitaka Halmashauri za Wilaya mkoani humo kuhakikisha hazipati hati chafu za ukaguzi wa fedha za serikali, vinginevyo wakurugenzi watendaji na watumishi katika ngazi hizo wasioweza kutekeleza agizo hilo waache kazi.

 

 

Mwasa aliyekuwa akizungumza na Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, alionyesha kukerwa na utendaji mbovu wa baadhi ya watumishi katika idara mbalimbali za halmashauri hizo, hali inayosababisha zipate hati chafu.

“Fedha zote za serikali zinazotumwa kwenye halmashauri lazima zitumike zilivyokusudiwa, vinginevyo watakaokiuka matumizi yake wawe tayari kuacha kazi,” alisema.

Namfahamu vizuri Mwasa niliyefanya naye kazi kampuni moja, ofisi moja na dawati moja akiwa bosi wangu anayesimamia na kupitisha maandishi yangu yote.

Naujua utendaji kazi, upole, upendo, nidhamu, uaminifu, tabia yake ya kutotaka kujikweza, kutotaka makuu, kupokea na kusikiliza ushauri wowote huku pia akishauri, kutokorofishana na watu na kupenda kuwaelekeza wote waliopo chini yake bila kinyongo wala hasira, ili wafahamu majukumu yao na kuheshimu utendaji wao.

Akiwa mwandishi wa habari kitaaluma, Mwasa alikuwa mhariri wangu tulipokutana katika kampuni ya Business Times Limited jijini Dar es Salaam. Nilifanya naye kazi kwa karibu mwaka mzima hadi nilipoacha na kujikita zaidi katika mambo ya kisiasa.

Nafahamu ubadhirifu mkubwa kabisa wa fedha unaofanywa na watendaji mbalimbali wa serikali na taasisi zake, wakiwamo wa halmashauri za manispaa, miji na wilaya nchini.

Najua jinsi watu wanavyoshindana kujitafutia utajiri wa haraka haraka kutokana na madaraka wanayopewa, wakitumia nafasi hizo kuwa mitaji ya kuanzisha na kuendeshea biashara zao, na si kuzitumikia kwa juhudi na maarifa yao yote, uadilifu na maendeleo ya sasa na yajayo ya nchi yetu.

Nimefuatilia kwa karibu matukio mengi yanayohusu wizi huo na ubadhirifu mwingine mwingi unaofanywa na watumishi hao wa umma, na pia nimefuatilia kwa karibu ili kujua hatua gani huchukuliwa ili kulikabili wimbi kubwa la mchwa wanaotafuna fedha za umma.

Nimelinganisha hatua zote hizo na kugundua bila mashaka yoyote kuwa wizi huo unatokana kwa kiasi kikubwa na mchwa hao kutofanywa chochote. Pili wakishtakiwa bado hawaoni kesi zao zikitoa majibu yanayoweza kuwa dawa madhubuti ya kuwadhibiti.

Tumeambiwa mara kadhaa kuwa wakurugenzi na watumishi wengine wa ngazi mbalimbali wa halmashauri za manispaa, wilaya na miji wameshitakiwa mahakamani wakikabiliwa na kesi za wizi, ubadhirifu au upotevu wa fedha za serikali, lakini hatuoni chochote kikiendelea baadaye.

Kwa mfano, zipo kesi nyingi zimefunguliwa dhidi yao katika maeneo tofauti nchini, lakini zote hazionyeshi mwelekeo wowote unaoweza kuwa dawa ya kero na matatizo mbalimbali waliyonayo wananchi huku wahusika wachache wakizidi kunufaika nazo.

Wapo wanaofanya ubadhirifu katika eneo moja na kuhamishiwa kituo kingine cha kazi, hivyo inawezekana kwamba wakichoka au kutaka kuhamia sehemu mpya wanaiba, kufanya ubadhirifu wa fedha za umma au kosa jingine lolote la utumishi kwa vile tayari wanafahamu kwamba hawafungwi na hawafukuzwi kazi.

Kama nilivyoweka wazi hapo mwanzo, hata wanaopata mkosi wa kushitakiwa mahakamani nao kesi zao huwa kama za kudanganyia watu au za maigizo.

Zinabaki zikitajwa huko kwa miaka mingi si kwa uzembe wa mahakama, bali kunatokana na walalamikaji ambao ni serikali kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Jeshi la Polisi kutotaka kuzimaliza ili walipa kodi wasahau.

Wanafungua kesi hizo kabla ya kufanya upelelezi yakinifu na kupata ushahidi madhubuti ili zikifika mahakamani iwe rahisi kusikilizwa mfululizo. Hali hii ingeliwezesha ziwe zinamalizika angalau katika muda usiozidi miezi 18 na kutolewa hukumu.

Nimesema namfahamu vizuri Mkuu wa Mkoa wa Tabora kwa sababu nimefanya naye kazi kampuni moja, ofisi moja na gazeti moja akiwa bosi wangu, na kisha nikataja sifa zake hasa za msingi zikiwamo zinazoweza kumfanya asimamie kikamilifu agizo lake au akashindwa.

Najua uchapakazi na utendaji wake, na pili nafahamu ni kiongozi mwenye uwezo mkubwa – anapenda wanaokuwa chini yake watekeleze majukumu yao kwa makini, ubora na uadilifu wote unaopaswa kuwapo.

Nauelewa upole na upendo wake, yule asiyetaka mtu yeyote aharibikiwe na chochote, jambo linaloweza kumuwia vigumu kuwachukulia hatua madhubuti watumishi wanaoharibu kazi za serikali na wizi wa fedha za umma.

Upole na upendo wake huo kwa watu unaweza kuwa ni kikwazo kwake hasa pale mkosaji anapokuwa mkubwa kwake kiumri, mambo ambayo akishindwa kuyadhibiti katika uongozi wa serikali atabaki anapiga kelele bila kumwajibisha yeyote.

Ataendelea kuzungumzia ukumbini na kushindwa kuchukua hatua zozote, nafasi inayoweza kutumiwa vizuri na wahusika kuendeleza wizi huo wa fedha za serikali, halafu halmashauri za mkoa huo zikazidi kupata hati chafu ambazo amesema hatazitaki.

Pamoja na upole na upendo wake huo, bado ninaamini hatakubali ageuzwe kuwa mbuzi wa kafara kwa kuwahurumia wakosefu, wale ambao hawapendi kutimiza wajibu wao – iwe kwa nidhamu, ubora na hata uadilifu wa hali ya juu.

Hapo ndipo nalazimika kungoja utekelezwaji au kupuuzwa kwake na “mchwa” wanaoweza wakaendelea kutafuna fedha za serikali katika halmashauri za mkoa huo za Urambo, Nzega, Sikonge, Uyui, Igunga, Tabora na Kaliua.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa Simu Na. 0762 633 244


By Jamhuri