Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Ajira kwa Watanzania katika miradi ya madini zimeendelea kuongezeka kwa kasi, zikipanda kutoka ajira 6,668 sawa na asilimia 95 mwaka 2018 hadi kufikia ajira 18,853 kati ya ajira 19,356 sawa na asilimia 97 kufikia Desemba 2024, mafanikio yanayoonesha mwelekeo chanya wa Serikali katika kulinda na kukuza maslahi ya wazawa kwenye Sekta ya Madini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 5, 2026 jijini Dodoma, Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema ongezeko hilo limetokana na utekelezaji madhubuti wa sera, sheria na kanuni za ushirikishwaji wa Watanzania (Local Content), sambamba na jitihada za Serikali kuhakikisha rasilimali madini zinawanufaisha wananchi moja kwa moja kupitia ajira na fursa za kiuchumi.

Amesema katika kuimarisha zaidi ushiriki wa Watanzania, Serikali kupitia Wizara hiyo imefanya marekebisho ya Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania za mwaka 2018, ambapo sasa kupitia Kanuni ya 13A, Serikali itakuwa ikitangaza mara kwa mara orodha ya bidhaa na huduma zitakazotakiwa kutolewa na kampuni za Kitanzania zinazomilikiwa kwa asilimia 100 na Watanzania.

Waziri Mavunde amesema, katika awamu ya kwanza, Tume ya Madini ilitangaza tarehe 14 Novemba, 2025 orodha ya bidhaa na huduma zinazopaswa kutolewa na kampuni hizo, hatua inayolenga kuongeza wigo wa ajira, utoaji wa huduma na ushiriki wa wazawa katika miradi ya madini kwa manufaa mapana ya Taifa.

“Nitumie nafasi hii kutoa rai kwa Watanzania kuendelea kuhakikisha wanapata utaalamu sahihi unaohitajika katika shughuli za madini ili wawe miongoni mwa wanaostahili kupatiwa fursa za ajira migodini sambamba na fursa za utoaji huduma katika miradi hiyo,” amesema Mavunde.

Aidha amewataka pia watoa huduma kuzingatia viwango stahiki ili kuendelea kuaminika huku akisisitiza kuwa wawekezaji wote wanapaswa kuzingatia Sheria ya Madini, Sura ya 123 pamoja na utekelezaji wa Kanuni za Local Content, na Watanzania wakihimizwa kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta hiyo ili kukabiliana na changamoto ya ajira na kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Ameeleza kuwa Serikali pia imeendelea kuweka utaratibu wa kisheria wa urithishwaji wa Watanzania katika nafasi zilizokuwa zikishikiliwa na wataalamu wa kigeni, ili kujenga uwezo wa kitaaluma na kuongeza idadi ya wazawa katika nafasi za uongozi kwenye kampuni za uchimbaji wa madini wa kati na mkubwa.

Ametolea Mfano wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaomilikiwa na Kampuni ya Twiga Minerals Corporation (Barrick Gold), ambapo kwa sasa nafasi zote za juu za uongozi zinashikiliwa na Watanzania.

Katika eneo la mapato,amesema jitihada hizo zimechangia ongezeko la makusanyo ya Serikali kutoka Sekta ya Madini, yakiongezeka kutokaShilingi bilioni 526.722 mwaka 2020/2021 hadi kufikia Shilingi trilioni 1.071 mwaka 2024/2025.

“Kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Wizara imepangiwa kukusanya Shilingi trilioni 1.2, ambapo hadi Desemba 31, 2025, jumla ya Shilingi bilioni 653.139 zilikuwa tayari zimekusanywa, sawa na asilimia 108.86 ya lengo la kipindi cha miezi sita, ” amesema.

Katika kuhakikisha Watanzania wananufaika zaidi na ajira na fursa za kiuchumi, Waziri Mavunde amesema Wizara hiyo kupitia Tume ya Madini imeimarisha usimamizi wa manunuzi migodini kwa kutoa kipaumbele kwa kampuni za Kitanzania.

Amesema hatua hiyo imeongeza thamani ya manunuzi ya bidhaa na huduma kutoka Shilingi trilioni 1.85 mwaka 2018 hadi kufikia Shilingi trilioni 4.41 mwaka 2024, sawa na asilimia 88 ya manunuzi yote.

“Serikali imehamasisha ujenzi wa viwanda vinavyozalisha bidhaa zinazohitajika kwa wingi migodini, hali iliyochochea uwekezaji wa kampuni za Kitanzania zikiwemo Rock Solutions Limited, Max Steel na East Africa Conveyors Supplies Limited, ambazo zimejenga viwanda kwa kushirikiana na wazalishaji wa kimataifa, huku bidhaa zikisambazwa ndani na nje ya nchi ikiwemo Tanzania, “ameeleza.

Pamoja na hayo amezungumzia kuunganisha Sekta ya Madini na sekta nyingine za uchumi kuwa Tume ya Madini imeanzisha Majukwaa ya Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini yanayoendeshwa kila mwaka, yakihusisha wamiliki wa leseni, watoa huduma, wasambazaji wa bidhaa migodini, taasisi za Serikali pamoja na Wizara ya Madini na taasisi zake.

Amesema hadi sasa, majukwaa manne yamefanyika kwa mafanikio makubwa, yakilenga kuboresha utekelezaji wa Local Content na kuongeza manufaa ya Sekta ya Madini kwa Watanzania na Taifa kwa ujumla.