Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Kondoa

Mtu mmoja anashikiliwa na Jeshi la Polisi wilaya ya Kondoa Mkoani Dodoma baada ya kukamatwa akiing’oa bendera na mabango ya Chama cha Wananchi (CUF) .

Hayo yamejiri wakati wa mapokezi ya Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa, Othman Dunga Machi 7, 2025, Wilayani Kondoa kitendo kinacho tafsiriwa kuwa ni kinyume cha sheria.

Mjumbe wa Kamati Tendaji CUF wilaya ya Kondoa, Ayubu Hamisi, amezungumza na Jamhuri Media kuwa watuhumiwa hao wanaosadikiwa kuwa ni wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambapo walivamia mitaani na kung’oa bendera 13 na mabango 25 ya CUF.

Amesema baada ya msako, walimkamata kijana mmoja ambaye alikiri kufanya uhalifu huo, na sasa anashikiliwa na Jeshi la polisi wilayani Kondoa.

Kutokana na hali hiyo Wanachama wa CUF wamesikitishwa na kitendo hicho na kueleza kuwa si cha kiungwana kwani Tanzania ni nchi yenye itikadi za vyama vingi hivyo ni vyema Sera za vyama zikahusika na sio kuhujumiana.

Hadija Selemani mwanachama wa CIF amesema kuwa,”Tukiwa tunajiandaa kwa sherehe ya kumpokea kiongozi wetu tumeshangazwa na tukio la kung’olewa kwa bendera na mabango,kwa kweli jambo hili limeleta taharuki,”amesema.

Naye Nssoro Junguke amekosoa vitendo vinavyohatarisha amani na kusema kuwa ni kinyume na siasa za kistaarabu ambazo Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akizitetea.

Wakati huohuo, Makamu Mwenyekiti wa CUF Taifa, Othman Dunga, amesema kuwa tukio hili ni la pili, baada ya tukio kama hilo kutokea Julai mwaka jana wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba.

Dunga amesisitiza kuwa bendera ni alama ya chama, na kwamba CUF itahakikisha inajenga ufuasi kwa kutafuta wanachama wapya.

Hata hivyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi, ameeleza kuwa taarifa kamili za tukio hili bado hazijamfikia, lakini anafuatilia suala hilo kwa karibu.