Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kilimanjaro
Licha ya kuhukumiwa kifungo cha miezi sita jela kwa kosa la kutishia kuua kwa panga, Albert Midimito, maarufu kwa jina la Chemli, amerudi kijijini na kuibua mgogoro mpya wa ardhi unaohusisha familia yake, huku mjane wa mdogo wake akidai kunyanyaswa.
Chemli alihukumiwa na Mahakama ya Mwanzo Kibosho Kindi Agosti 28, 2024 katika Kesi Namba 120/2024, kwa kosa la kutishia kuua kinyume cha Kifungu cha 89(2)(b) cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16, Marejeo ya 2022.
Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mwandamizi, Adam Melchior, aliyedai kuwa kwa mujibu wa sheria, kifungo hicho hufanyika kwa hesabu ya mchana pekee, hivyo kuwa sawa na miezi sita.
Chemli anadaiwa kutenda kosa hilo Juni 30, 2024 katika Kijiji cha Sisamaro, Kibosho Okaoni, ambapo aliwatishia kwa panga ndugu zake waliokwenda kwake kutafuta suluhu ya mgogoro wa ardhi baina yake na mke wa mdogo wake aliyefariki dunia mwaka 2010, akiacha mjane na watoto wanne.
Licha ya kifungo, Chemli ameripotiwa kuendelea na msimamo mkali dhidi ya familia, na kuibua hali ya taharuki alipolazimisha kikao cha ukoo kifanyike nyumbani kwake, jambo lililopingwa na ndugu waliodai kuwa awali alikwisha kuwatishia kuwaua kwa panga.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Sisamaro, Sarutari Mwanga, amesema Chemli alimfuata kwa malalamiko kuhusu mipaka iliyowekwa shambani kwake akiwa gerezani, lakini alipoitisha kikao cha familia, Jumamosi Mei 24, 2025 alionekana kutokuwa tayari kwa suluhu.
“Nikamwambia nitaiita familia, wakafika, lakini badala ya kutafuta amani, akaanza kuuliza nani kaweka mipaka na kusababisha mabishano kati yetu. Nikamweleza kuwa amani ndiyo msingi wa kutatua migogoro kama hii, lakini hakuwa tayari,” amesema Mwanga.

Makamu Mwenyekiti wa ukoo wa Nchau, Cosmass Mallya, amesema walihudhuria kikao wakiamini ni cha msamaha, lakini walishangazwa na mabadiliko ya ajenda.
“Chemli ametusumbua kwa muda mrefu. Tulidhani anakuja kutuomba msamaha na kuikabidhi familia mali ya mjane, lakini alikuja na madai ya mipaka. Tumesema hatupo tayari, tutaendelea na kesi mpaka haki ipatikane,” amesema Mallya.
Mjane anayedai kunyanyaswa, Anna Mathius Midimito, amesema maisha yake yamekuwa ya hofu tangu mume wake afariki dunia kutokana na vitisho kutoka kwa Chemli.
“Niliwahi kukimbilia porini na watoto wangu baada ya kutishiwa. Na hata sasa, bado anatunyanyasa. Anadai masare ya mipaka (majani) na migomba imepandwa kwenye shamba lake, lakini si kweli,” amesema Anna.
Akijibu tuhuma hizo, Chemli amesema anatafutwa na familia yake kwa lengo la kumdhuru na kwamba kikao hicho kilikuwa ni cha kutaka kufahamu aliyeweka mipaka, si kuomba msamaha.
“Hii ni vita. Wananitafuta kunidhuru, sitaki kesi mimi. Kama ni kwao basi waniambie, lakini siyo kuniandalia vikao vya kunifukiza,” amesema Chemli.
Katibu wa Usuluhishi wa Migogoro wa Kata ya Kibosho Okaoni, Bakari Kaniki, amesema serikali imeshaingilia kati mgogoro huo na kupanga kikao rasmi kufanyika Jumanne ijayo.
“Jana tulikuwa eneo la tukio, na kabla ya hapo nilikwenda kuona. Kweli kuna haki imekiukwa. Pale palitakiwa mamlaka husika zisikilize mgogoro. Tulikubaliana na mtendaji wa kijiji kwamba kikao kitafanyika Jumanne. Kesi haziwezi kufanyika ovyo ovyo kwenye maeneo ya tukio wakati serikali ina ofisi za kutolea haki,” amesema Kaniki.