Mahakama ya kijeshi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imemhukumu kifo aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Joseph Kabila, bila mwenye kuwepo, baada ya kumtia hatiani kwa makosa kadhaa mazito yakiwemo usaliti na uhalifu dhidi ya binadamu.

Hukumu hiyo imetolewa Jumanne na Luteni Jenerali Joseph Mutombo Katalayi, aliyesimamia shauri hilo katika mji mkuu Kinshasa. Jaji huyo alisema Kabila, mwenye umri wa miaka 54, amepatikana na hatia katika mashtaka yanayojumuisha usaliti, mauaji, unyanyasaji wa kingono, mateso na uasi.

Kabila, ambaye aliitawala DRC kuanzia mwaka 2001 hadi 2019, aliondoka nchini humo mwaka 2023. Hata hivyo, mwezi Mei mwaka huu alionekana kwa muda mfupi katika maeneo ya mashariki ya nchi hiyo yanayodhibitiwa na waasi wa M23.

Kwa sasa haijulikani alipo baada ya hukumu hiyo ya mahakama ya kijeshi.

Mwendesha mashtaka alimshtaki Kabila kwa kuunga mkono waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda, ambao mwaka huu wametwaa maeneo makubwa ya mashariki yenye utajiri wa madini. Kesi yake ilianza kusikilizwa bila ya yeye kuwepo tangu Julai.

PPRD: Kesi hii imechochewa kisiasa

Waendesha mashtaka walisema Kabila alijenga usuhuba na M23 kwa lengo la kuipindua serikali ya Rais Felix Tshisekedi na kurejesha ushawishi wake wa kisiasa.

Kabila, kwa upande wake, amewahi kulaani mashitaka hayo akiyaita “kesi ya maigizo” na kuushutumu mfumo wa mahakama nchini kwa kuwa “chombo cha ukandamizaji”.

Aliongeza kuwa kesi dhidi yake, pamoja na kukamatwa kwa maafisa waandamizi wa kiraia na kijeshi, ni ishara ya kile alichokiita mgogoro wa kina wa uongozi, haki na mwelekeo wa taifa.

Chama chake, People’s Party for Reconstruction and Democracy (PPRD), kimesema hukumu hiyo ni uwindwaji wa kisiasa na njama ya kumwondoa mpinzani mkubwa wa serikali.

Kabila akutana na viongozi wa kidini huko Goma

“Wote wanajua kuwa hukumu ya Rais wa heshima Joseph Kabila Kabange ilishapangwa na serikali ya sasa. Kinachoendelea ni maigizo tu,” alisema katibu wa chama hicho, Emmanuel Ramazani Shadary.

Katika mji mkuu Kinshasa, viongozi wengine wa PPRD pia wameripotiwa kushinikizwa na vyombo vya dola, huku baadhi wakiitwa na waendesha mashtaka na wengine kukamatwa, jambo linaloongeza mvutano wa kisiasa.

Chanzo: Mashirika