Mfanyabiashara Khamis Lowongo (Meshack) mwenye umri wa miaka 38 anayetuhumiwa kumuua mke wake, Naomi Marijani, kwa kumchoma moto akitumia magunia mawili ya mkaa Kigamboni, jijini Dar es Salaam amekuwa na vituko mbalimbali kila afikapo mahakamani.

Mtuhumiwa huyo kwa mara ya kwanza alikamatwa na Jeshi la Polisi baada ya Gazeti la JAMHURI Julai 16, mwaka huu kuandika habari kuhusiana na uwezekano wa kuuawa kwa Naomi baada ya mume wake kudai kuwa ametoweka. Habari hiyo ilipoandikwa Jeshi la Polisi nchini lilitangaza kumkamata mume wa Naomi ambaye baadaye alikiri kumuua mke wake kisha kumchoma moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa.

Julai 17

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam lilitangaza kumkamata Meshack ambaye baada ya mahojiano alikiri kumuua Naomi kisha kumteketeza kwa moto huko shambani kwake.

Julai 18 

Viongozi mbalimbali likiwemo Jeshi la Polisi walitembelea nyumbani kwa Naomi Kigamboni pamoja na mahala ambapo anasadikika kufukiwa.

Julai 31

Khamis Luwongo (Meshack) alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza kwa tuhuma za mauaji ya kukusudia.

Meshack alipanda kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi, Salum Ally na kusomewa mashitaka na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, aliyesema mshitakiwa ni mfanyabiashara anayeishi Gezaulole, Kigamboni.

Wankyo amesema mshitakiwa anatuhumiwa kumuua mkewe Naomi Marijani (36), Mei 15, mwaka huu. Mshitakiwa hakutakiwa kujibu lolote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Upelelezi wa kesi hiyo unaendelea ambapo mshitakiwa alipelekwa gerezani hadi Agosti 13, mwaka huu kesi hiyo ilipotajwa.

Agosti 13 

Siku hii ilikuwa siku ya kioja cha kwanza kwa Khamis. Kesi yake ilipotajwa mbele ya Hakimu Mkazi Salum Ally, alinyoosha mkono na kuomba kuzungumza jambo, hali iliyoifanya mahakama nzima kukaa makini kusikiliza alichotaka kuzungumza.

Aliporuhusiwa alisema: “Mheshimiwa, nina kitu ambacho nataka nikueleze kuhusu waandishi wa habari. Wamekuwa wakinipiga picha kuanzia chini hadi ndani ya mahakama, sasa nakueleza hivi, nitakuja kuishangaza mahakama, nitafanya kitu kibaya sana.”

Akionyesha kukerwa na kitendo cha kupigwa picha mara kwa mara alisema kwamba kesi hiyo inamuumiza kichwa na hajui mwisho wake utakuwaje na waandishi wanapompiga picha wanazidi kumuondolea utulivu wa akili, hivyo hataki kupigwa picha.

“Kuna kesi ambayo inanikabili na sielewi hatima ya kesi yangu. Hapa nilipo kichwa changu kimevurugika, nina mawazo ya mtoto wangu na ninapofika hapa ili akili yangu itulie wanakuja kunipiga picha. Sasa nawaeleza kuwa nitafanya kitu kibaya ambacho mahakama haitatarajia,” alisema.

Wakili wa Serikali akijibu onyo lililotolewa kwa waandishi wa habari, Wakili Wankyo alimueleza Khamis kuwa kupigwa picha ni hali ya kawaida na washitakiwa wote wanaofikishwa mahakamani wanapigwa picha, hivyo awape uhuru waandishi wa habari wafanye kazi yao kwa uhuru.

“Lengo la waandishi wa habari ni kutoa habari na kuwajuza wananchi, hivyo kumbuka hii ni mahakama na hatujui kitu unachotaka kufanya ni kitu gani,” alidai Wankyo.

Hakimu Ally baada ya kusikiliza hoja hizo, aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 27, kwa ajili ya kutajwa na mshitakiwa kurudishwa rumande.

Agosti 27

Kutokana na Khamis kuwa mwingi wa vioja, siku hii alifika mahakamani akiwa amejifunga usoni kitambaa cha kufutia jasho, maarufu kama ‘handkerchief’ kuficha sura yake. Pamoja na mtindo huo mpya alioubuni, pia alikuwa na ombi jipya kwa hakimu kuwa apatiwe ‘line’ zake mbili za simu zenye zaidi ya Sh Milioni 5 kwa ajili ya matumizi ya nyumbani kwake pamoja na kumlipia ada mwanae Gracious.

Khamis ambaye alifikishwa mahakamani hapo akiwa na pingu miguuni kutokana na vitisho alivyotoa hapo awali kwa waandishi wa habari kwamba atawafanya kitu kibaya, alitoa ombi hilo mbele ya Hakimu Mkazi, Salum Ally.

Mshitakiwa alitoa maombi hayo baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, kusema kuwa kesi hiyo leo imeitishwa kwa ajili ya kutajwa, upelelezi bado haujakamilika.

Baada ya kueleza hayo, Said alinyoosha mkono na ndipo alipoanza kumueleza hakimu kwamba ana mambo mawili muhimu ikiwemo nakala yake ya hati ya mashitaka na ‘line’ zake za simu zilizopo Kituo Kikuu cha Polisi (Central) na kuomba apatiwe ‘line’ hizo zenye zaidi ya Sh milioni 5 zitumike kwa matumizi madogo madogo na kumlipia ada ya mtoto wake.

“Sitaki simu, ila naomba nipatiwe ‘line’ nimpatie ndugu yangu atoe hizo hela kwa ajili ya matumizi, ikiwezekana zitolewe hata polisi wakiwepo,” alisema.

Baada ya kueleza hayo, Wakili Wankyo alisema simu hizo ni sehemu ya upelelezi, hivyo kwa sasa itakuwa vigumu kumpatia, kwa sababu hawawezi kuamini moja kwa moja kama kweli anahitaji kutoa hizo hela.

“Nakumbuka nakala ya hati nilishampa, ila haina shida, nitampa tena leo, lakini kuhusu kupewa simu ili atoe pesa hilo haliwezekani kwa sababu zilichukuliwa kama vielelezo vya upelelezi, hivyo avumilie tu kwa sababu hatuwezi kumpa simu wala laini mpaka upelelezi utakapokamilika,” alisema Wankyo.

Hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi leo Septemba 10, mwaka huu itakapotajwa tena, na mshitakiwa amerudishwa rumande.

Kwa mujibu wa sheria ya Tanzania, Kanuni ya Adhabu Sura ya 20, Kifungu cha 197, kosa la kuua kwa kukusudia adhabu yake ni kifo. Hivyo, ikiwa Luwongo atapatikana na hatia ya kumuua Naomi kwa kukusudia, atanyongwa hadi kufa.

Kamanda wa Polisi (RPC) wa Temeke, Amon Kakwale, alitoa taarifa kwa umma ikielezea namna Luwongo alivyokiri kumuua mkewe huyo, iliyosema: “… kosa mauaji. Mtoa taarifa ni SP. Thobias Walelo, Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kigamboni. Anaeleza kuwa mnamo tarehe 15. 07. 2019 majira ya saa 08:00 hrs huko Gezaulole, Kata ya Somangila, Wilaya ya Kigamboni, Jiji la Dar es Salaam, nyumbani kwake Khamis Said Luwongo (38), Makonde, mfanyabiashara, mkazi wa Gezaulole anaeleza alimpiga na kumuua mke wake aitwaye Naomi Orest Marijani (36), Mpare, mfanyabiashara na mkazi wa Gezaulole.

“Mara baada ya mauaji hayo, Khamis Said Luwongo anaeleza kwamba alichukua mwili wa mke wake na kuuweka kwenye shimo alilochimba kwenye banda lake la kufugia kuku, kisha aliweka mkaa gunia mbili na mafuta ya taa, kisha akawasha moto uliowaka muda mrefu na mwili wote kuteketea kuwa majivu.

“Kisha alichukua majivu hayo akaweka kwenye mfuko na kubeba kwa kutumia gari lake lenye namba T 206 CEJ aina ya Subaru Forester, rangi nyeusi na kuupeleka kwenye shamba lake lililoko Kijiji cha Marogoro, Kata ya Vikindu, Wilaya ya Mkuranga, Mkoa wa Pwani.

“Alichimba shimo kwenye shamba lake kisha kuweka hayo majivu na kufukia na akapanda mgomba juu yake. Kisha Khamis Said Luwongo alikaa nyumbani kwake akisema mke wake ametoroka nyumbani, tarehe 19. 05. 2019 alifungua taarifa ya mke wake kutoroka nyumbani na kupewa RB ya Kituo Kidogo cha Polisi, Mjimwema, MJ/RB/234/2019 yahusika. Kisha kuwajulisha ndugu, jamaa na marafiki zake kuwa mke wake ametoroka nyumbani.

“Tarehe 12. 06. 2019 alifungua jalada KGD/IR/3617/2019 kosa kutelekeza mtoto. Akimtuhumu mke wake kuwa ametelekeza mtoto aitwaye Gradous (sahihi Gracious) Khamis mwenye umri wa miaka sita. Tarehe 13. 06. 2019 ndugu wa Naomi Orest Marijani walitoa malalamiko yao ya kupotea kwa ndugu yao kukafunguliwa jalada la uchuguzi Temeke/CID/PE/69/2019 yahusika.

“Upelelezi uliendelea Khamis Said Luwongo akiwa anakwenda kuripoti Ofisi ya RCO Temeke hadi tarehe 15. 07. 2019 Khamis Said Luwongo alizuiliwa na mahojiano ya kina kufanyika ndipo akaamua kusema ukweli kuwa alimuua mke wake, tarehe 16. 07. 2019 aliongoza timu ya makachero kutoka Kanda Ofisi ya ZCO, Ofisi ya RCO Temeke, wataalamu kutoka PHD na daktari, iliyokuwa inaongozwa na ASP Msisiri OCS Kigamboni.

 “Walifanikiwa kupata mabaki ya mwili yamechukuliwa kwenda Kanda kwa ajili ya uchunguzi zaidi. Chanzo cha mauaji ni wivu wa kimapenzi, tukio limekaguliwa na SP Thobias Walelo, OC CID Kigamboni akishirikiana na makachero. Upelelezi unaendelea, nitaendelea kukujulisha maendeleo.”

Ofisi ya Mkemia Mkuu ilifanya uchunguzi wa vinasaba vya damu, ambapo taarifa zilionyesha kuwa mabaki ya mwili yaliyopatikana ni ya Naomi.

727 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!