Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Aprili 5,2026 Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, alishiriki Tamasha la Pasaka la Mtoko na Christina Shusho lililofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Katika tamasha hilo, Waziri Mkuu alisema kuwa Pasaka ni kipindi muhimu kinachowakumbusha Watanzania kuishi kwa upendo, mshikamano na kudumisha amani katika jamii.
“Amani si kwa ajili ya faida ya Rais wala Serikali, bali ni kwa ajili ya kila mwananchi. Pasipo amani hata shughuli ndogo kama kujitafutia kipato haziwezi kufanyika.” alisema.
Alisema kuwa mnufaika wa kwanza wa amani ni mwananchi mwenyewe, kwani bila utulivu hata shughuli za kiuchumi, kijamii na ibada haziwezi kufanyika ipasavyo.
Aidha, amempongeza mwimbaji wa muziki wa Injili, Christina Shusho, kwa kuandaa tamasha hilo kubwa lililovuta maelfu ya waumini, akisema mafanikio yake yanaonesha kuwa lina kibali cha Mungu.
“Ukiona jambo linafanikiwa kiasi hiki, ujue lina kibali cha Mungu. Serikali haitakuwa kikwazo katika mipango ya kuendeleza huduma ya injili.” alisema.

Hata hivyo Watanzania ni vyema wakaendelea kuisimamia misingi ambayo imelifanya taifa hili kuwa kioo
cha amani na utulivu duniani. Tanzania imejijengea msingi imara wa amani tangu uhuru wake chini ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye alikuwa Rais wa Tanzania wa Awamu ya Kwanza.
Kupitia falsafa ya umoja, ujamaa na kujitegemea, aliweka misingi ya taifa lisilobagua kwa misingi ya kabila, dini au itikadi hivyo bado tuna wajibu Watanzania kuendelea kusimamia na kufuata falsafa hizo ambazo ni nguzo zetu ambazo zimeendelea kuwa kioo cha amani Afrika na duniani.
Tukumbuke kuwa vipindi mbalimbali vya Serikali zinazoongoza zimeendelea kuenzi urithi huo kwa kusisitiza amani, utulivu, maridhiano na mshikamano wa kitaifa pale changamoto ndogondogo zinapojitokeza katika nyakati tofauti kwa kushirikiana kwa maridhiano na kutatuliwa.
Katika kuendelea kulinda tunu hizo, ni vyema sasa Watanzania wakawa macho dhidi ya watu ama makundi yenye nia ovu ya kuchochea ama kuhamaisha vurugu kwa maslahi yao binafsi kwani migogoro huanzia kwa njia mbalimbali mfano kauli za uchochezi, upotoshaji na hata propaganda zenye nia ya kugawa jamii na kuleta chuki inayoweza kuzaa matunda mabaya.
Oktoba 29, 2025 wakati wa Uchaguzi Mkuu tulishuhudia yaliyotokea, ambayo hatutamani yarudie tena, badala yake ni wakati wa kuendelea kushirikiana na kuongeza juhudi katika mapambano ya kujenga uchumi wa Tanzania lakini pia wa kila mmoja mmoja.
Hivi sasa tunashuhudia baadhi ya mataifa yakiwa katika hali ya kuhudhunisha sana, watu wakipoteza maisha bila ya hatia, lakini uharibifu mkubwa wa miundombinu ambayo chanzo chake yalianza maneno maneno na mwishowe kuingia kwenye misukosuko zinazozigharimu nchi na hata dunia kiujumla.

Mataifa mengi yenye rasilimali nyingi yameingia kwenye misukosuko hiyo ambayo tunaweza kuita ni vita ya kiuchumi na kusababisha hasara kubwa si kwa ndani ya nchi lakini pia nje ya nchi.
Hivyo kwa pamoja Watanzania tuna wajibu wa kulinda amani na utuliu wa nchi ili kuendelea kulinda raslimali zetu, Tanzania ni kati ya nchi ambayo Mungu ameibariki kwa kuwa na utajiri kama madini , ardhi yenye rutuba, mbuga zenye wanyama wengi na wa kila aina ambao kwa dunia baadhi hupatikana Tanzania tu.
Lakini pia ina utajiri wa gesi asilia hivyo, kulinda amani na utulivu si tu kwa ajili ya mshikamano wa kijamii, bali pia kwa ajili ya kulinda rasilimali na mustakabali wa uchumi wa taifa. Mungu ibariki Tanzania na watu wake.
